Wanachama wa Daesh wahukumiwa kifungo cha miaka 35 Malaysia
(last modified Fri, 31 Mar 2017 06:40:44 GMT )
Mar 31, 2017 06:40 UTC
  • Wanachama wa Daesh wahukumiwa kifungo cha miaka 35 Malaysia

Wanachama wawili wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) ambao pia walihusika katika shambulizi dhidi ya klabu ya usiku nchini Malaysia, wamehukumiwa kifungo cha miaka 35 na mahakama kuu ya nchi hiyo.

Akitoa hukumu hiyo, jaji Nurudin Hassan, aliyekuwa akisimamia faili hilo amesema kuwa, Imam Wahyudin Karjono mwenye umri wa miaka 22 na Jonius Ondie Jahali mwenye umri wa miaka 25, walihusika katika utegaji bomu lililozusha hofu na wasi wasi mkubwa, sambamba na kujeruhi watu wengine wanane.

Imam Wahyudin Karjono na Jonius Ondie Jahali 

Jaji Nurudin Hassan amemhukumu kifungo cha miaka 25 kila mmoja kwa kosa hilo la utegaji bomu huku akiwahukumu pia kifungo cha miaka 10 kila mmoja kutokana na kuwa wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh nchini Malaysia. Ameongeza kuwa, mahesabu ya vifungo vyao yanaanza tangu tarehe waliyotiwa mbaroni yaani katikati ya mwaka jana.

Ukumbi ambao vijana hao walishambulia kwa bomu mwaka jana

Imam Wahyudin Karjono, alikuwa mfanyakazi wa kiwanda kimoja nchini humo na Jonius Ondie Jahali hakuwa na ajira. Wote wawili walikuwa wakijishughulisha na harakati za kigaidi ambapo mwaka jana walifyatua bomu katika kilabu ya usiku katika jimbo la Selangor nchini humo. Kadhalika vijana hao wanatuhumiwa kwa kuendesha harakati pana za kigaidi nchini Malaysia kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram.