Lavrov: Marekani imevuruga mchakato wa kisiasa wa Syria
Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa mashambulizi ya makombora ya Marekani huko Syria yamekwamisha kutatuliwa mgogoro wa Syria kwa njia za kidiplomasia.
Sergei Lavrov amesema katika mkutano na waandishi wa habari huko Moscow mji mkuu wa Russia akiwa na Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Senegal, Mankeur Ndiaye kuwa, mashambulizi ya makombora ya Marekani dhidi ya kituo cha jeshi la anga huko Syria yameifanya hali ya mambo kuzidi kuwa mbaya na wakati huo huo mashambulizi hayo yamekwamisha jitihada za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria kwa njia za kisiasa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameashiria namna baadhi ya pande za kieneo na kimataifa zinavyofanya jitihada ili kunufaika na hali mbaya ya mambo ya sasa huko Syria na kuongeza kuwa Moscow imesisitiza mara kadhaa kwamba uchunguzi huru chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa unapasa kufanywa ili kuchunguza madai kuwa serikali ya Syria imetumia silaha za sumu za kemikali.
Lavrov amebainisha kuwa hivi sasa iwe ni wapinzani wa nje ama wa ndani huko Syria na pia pande nyingi husika katika eneo na kimataifa zinafanya kila ziwezalo ili kunufaika na hali ya mambo ya sasa iliyopo ili kuiarifisha serikali ya Rais Bashar Assad kuwa chanzo cha mgogoro huko Syria; jambo alilolitaja kuwa ni la hatari.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amevitaja vitisho vya Marekani dhidi ya Korea ya Kaskazini kuwa ni hatua isiyo sahihi na kueleza matarajio yake kwamba, hatua za upande mmoja zilizotelekezwa hivi karibuni huko Syria, hazitatekelezwa dhidi ya Korea ya Kaskazini.