Korea Kaskazini yasema itaiadhibu vikali Israel
Korea Kaskazini imesema itauadhibu vikali utawala haramu wa Israel kwa kuthubutu kuuvunjia heshima uongozi wa nchi hiyo.
Katika taarifa, Korea Kaskazini imuetaja utawala wa Israel kuwa 'mmiliki pekee haramu' wa silaha za nyuklia Mashariki ya Kati na hivyo kuwa tishio kwa usalama wa dunia.
Kauli hiyo ya wakuu wa Pyongyang imekuja baada ya Waziri wa Vita wa Israel Avigdor Lieberman kumtaja kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un kuwa eti ni "mwendawazimu" ambaye anasimamia, "kundi la watu wenye misimamo mikali" ambao "wanavuruga uthabiti wa dunia."
Katika kujibu matamshi hayo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini imesema Lieberman ni mtu duni na khabithi na kwamba madai yake ni sehemu ya propaganda za Israel zenye lengo la kufunika jinai zake. Aidha taarifa hiyo imeitaja Israel kuwa nchi ya kinafiki ambayo inavuruga usalama katika eneo.
Taarifa hiyo imesema Israel ndio mmiliki pekee haramu wa silaha za nyuklia Mashariki ya Kati na inafanya hivyo kwa himaya ya Marekani lakini wakuu wa Israel wanathubutu kupinga silaha za nyuklia za kujihami za Korea Kaskazini. Taarifa hiyo imesema Korea Kaskazini inamiliki silaha za nyuklia kwa malengo halali ya kujihami na kukabiliana na uchokozi wa Marekani. Pyongyang imeitaja Israel kuwa mhusika wa jinai dhidi ya binadamu na mkaliaji mabavu anaye lenga kudhibiti eneo na kuwakandamiza Wapalestina.