UN yatetea shirika lake linalohudumia wakimbizi wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i30420-un_yatetea_shirika_lake_linalohudumia_wakimbizi_wa_palestina
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuunga mkono shirika la umoja huo linalohudumia wakimbizi wa Kipalestina, baada ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kutoa wito wa kuvunjwa taasisi hiyo ya kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 13, 2017 09:32 UTC
  • UN yatetea shirika lake linalohudumia wakimbizi wa Palestina

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuunga mkono shirika la umoja huo linalohudumia wakimbizi wa Kipalestina, baada ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kutoa wito wa kuvunjwa taasisi hiyo ya kimataifa.

Farhan Haq, Msemaji wa UN amesema Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametiwa wasi wasi na matamshi ya hivi karibuni yaliyotolewa dhidi ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA) na uhalali wa operesheni zake.

Gutteres ameapa kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa UNRWA sambamba na kupongeza majukumu ya asasi hiyo ya kutoa huduma za msingi kwa mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina na vile vile kulinda haki zao.

Matamshi ya Katibu Mkuu wa UN ni radiamali kwa matamshi ya hivi karibuni ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, ambaye alitoa wito wa kuvunjwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA), linalowasaidia mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina.

Farhan Haq, Msemaji wa UN

Netanyahu aliituhumu UNRWA kuwa inaendesha kampeni za chuki dhidi ya Israel, zikiwemo shule zinazofadhiliwa na kuendeshwa na shirika hilo la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, wakati umefika wa kulivunja shirika hilo la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina na kuliunganisha na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR).

Sami Mshasha, Msemaji wa UNRWA hivi karibuni alisema mamlaka na majukumu ya asasi hiyo yako chini ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kwamba, hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuingilia utendaji wa taasisi hiyo.