Russia yawatahadharisha magadi kuhusu mashambulizi ya kichochezi ya kemikali huko Syria
Bi Maria Zakharova Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema leo Alhamisi kuwa Moscow ina taarifa kwamba magaidi wanapanga kufanya mashambulizi ya kemikali ya kichochezi huko Syria ili kuhalalisha mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya vikosi vya serikali ya Damascus.
Zakharova amesema kuwa, kulingana na taarifa zilizopo, makundi ya kigaidi huko Syria yanapanga kutekeleza mashambulizi ya kichochezi kwa kutumia gesi za kemikali zenye sumu ili kuhalalisha mashambulizi ya Marekani dhidi ya maeneo ya vikosi vya serikali ya Damascus. Ameongeza kuwa kundi la Daesh hivi sasa linahamisha vifaa vinavyotumika kutengenezea silaha, zikiwemo mada zenye gesi kutoka eneo la Raqqah hadi katika maeneo ya mkoa wa Deir-Zor yanayodhibitiwa na kundi hilo.
Afisa huyo wa Russia amesisitiza pia kwamba nchi yake itaomba kufanyike uchunguzi usioegemea upande wowote kuhusu shambulio la kemikali lililotekelezwa katika mji wa Khan Shaykhun tarehe Aprili mwaka huu na uchochezi mwingine wa kemikali unaoendelezwa dhidi ya serikali halali ya Syria.
Taarifa nyingine kutoka Syria zinasema kuwa mlipuko wa bomu umetokea leo katika kituo cha basi katika mji wa Hama magharibi mwa Syria na kuuwa watu wasiopungua wawili na kujeruhi wengine 11.