Nchi za Kiislamu zatakiwa kushirikiana kimataifa
Mwenyekiti wa Kundi la Urafiki la Mabunge ya Iran na Niger katika Bunge la Iran amesema kuna haja kwa nchi za Kiislamu kushirikiana katika uga wa kimataifa ili kuwa na taathira katika maamuzi muhimu kwa maslahi ya nchi za Kiislamu.
Mahdi Farshadan, Mwenyekiti wa Kundi la Urafiki la Mabunge ya Iran na Niger katika Bunge la Iran ameyasema hayo leo mjini Tehran alipokutana na kufanya mazungumzo na Massani Cornei, Mwenyekiti wa Kundi la Urafiki la Mabunge ya Iran na Niger katika Bunge la Niger. Ameashiria uhusiano wa kirafiki wa Iran na Niger katika kipindi cha miaka 30 iliyopita na kusema, kwa kuzingatia taathira ya makundi ya kirafiki ya mabunge katika kurahisisha uhusiano wa kirafiki baina ya nchi, Kundi la Urafiki wa Mabunge ya Iran na Niger liko tayari kuwa na nafasi katika kuboresha uhisiano wa nchi mbili katika sekta za uchumi, afya na utamaduni.
Naye Mbunge Massani Cornei wa Niger amesema Iran kama nchi ya Kiislamu inapewa umuhimu wa kipekee katika sera za kigeni za Niger. Aidha amesema Niger kama mwanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu inalipatia umuhimu suala la mshikamano na nchi za Kiislamu duniani.
Cornei anaongoza ujumbe wa wabunge kutoka Niger unaitembelea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa lengo la kuboresha uhusiano wa nchi mbili.