Aug 18, 2017 15:02 UTC
  • Iran yalaani shambulizi la kigaidi la Barcelona

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali shambulizi la kikatili na kigaidi lililotokea jana Barcelona huko Uhispania na kusema taifa la Iran linatoa mkono wa pole kwa serikali, taifa na familia za wahanga wa shambulizi hilo.

Bahram Qassemi amesemaq kuwa, ugaidi umekuwa tatizo la ulimwengu mzima na kuongeza kuwa, baada ya kupata kipigo katika medani za vita sasa wamagaidi wa Mashariki ya Kati wamehamishia mashambulizi yao katika maeneo mengine ya dunia na kulenga watu wa kawaida na wasio na hatia yoyote.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, matatizo ya dunia yanahitaji suluhisho la dunia nzima na kuongeza kuwa: Nchi zote zinazopenda amani na wale wenye nia ya kweli ya kupamabana ipasavyo na ugaidi wanapaswa kuunda muungano wa kimataifa wa kukabiliana na ukatili, machafuko na ugaidi na kulipa kipaumbele cha kwanza suala la kung'oa kabisa mzizi wa ugaidi.

Baadhi ya waathirika wa shambulizi la jana, Barcelona

Qassemi amesema kuwa, Iran ambayo ni miongoni mwa wahanga wa ugaidi na daima imekuwa mstari wa mbele kupambana na uovu huo iko tayari kusaidia na kushirikiana na jamii ya kimataifa katika medani ya kupambana na janga hilo. 

Watu 13 wameuawa na wengine 100 kujeruhiwa katika shambulizi la jana katika eneo la kitalii la Las Ramblas katikati ya jiji la Barcelona. Masaa machache baadaye kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza kuwa ndilo lililofanya shambulizi hilo. 

Tags