London yahofia kurejea Uingereza mamia ya magaidi kutoka Syria na Iraq
Waziri wa Nchi wa Usalama wa Ndani wa Uingereza ametahadharisha kuwa tishio la ugaidi dhidi ya nchi hiyo linaongezeka kufuatia kushindwa kundi la kigaidi la Daesh huko Iraq na Syria.
Ben Wallace amesema kuwa magaidi wa Daesh wamepoteza udhibiti wa mji wa Mosul kaskazini mwa Iraq na huku wakiukimbia pia katika mji Raqqah katikati mwa Syria. Amesema hatua hiyo inaweza kuwafanya magaidi wa Daesh kurejea Uingereza jambo ambalo litakuwa ni tishio kwa usalama wa nchi hiyo.
Ben Wallace ameongeza kuwa magaidi wanaweza kutumia gari au kisu kuwaulia watu kwenye mitaa ya Uingereza, hata hivyo akasema serikali ya nchi hiyo inaangalia namna ya kuzuia matukio hayo. Katika kipindi cha mwaka 2011 hadi 2016 zaidi ya magaidi mamluki 42,000 kutoka nchi 120 walielekea Iraq na Syria kujiunga na kundi la Daesh; ambapo zaidi ya 5000 miongoni mwao walikuwa raia wa nchi za Ulaya. Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Ulaya zinaonyesha kuwa asilimia 15 hadi 20 ya magaidi wameuliwa, asilimia 30 hadi 35 wamerejea katika nchi walikotoka na wengine karibu asilimia 50 wameendelea kuwepo huko Syria na Iraq.
Magaidi hao wengi wao wanatoka katika nchi za Ubelgiji, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Austria, Denmark, Finland, Uholanzi, Uhispania na Sweden. Nchi za Ulaya ikiwemo Uingereza ambazo hazijakoma kuchukua hatua za kuwasaidia magaidi katika eneo la Mashariki ya Kati khususan magaidi walioko huko Syria, hivi sasa zinakabiliwa na wimbi la magaidi hao wa nchi za Ulaya wanachama mwa Daesh wanaorejea katika nchi hizo huku zikiwa na wasiwasi pia wa kutekelezwa mashambulizi ya kigaidi na magaidi hao.