Iran yaipongeza IAEA kwa kupuuza mashinikizo ya US dhidi yake
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepongeza msimamo wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA wa kutoa ripoti isiyoegemea upande wowote sambamba na kupuza mashinikizo ya Marekani ya kuutaka ukague vituo vya kijeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Reza Najafi, Balozi wa Iran katika IAEA amesema msimamo wa wakala huo haukuegemea upande wowote, haujafuata mashinikizo na umechukuliwa kwa kufuata misingi ya utaalamu.
Kadhalika afisa huyo wa Iran ameeleza kushangazwa kwake na kitendo cha Marekani cha kutoa mashinikizo katika mambo ambayo hayana msingi pasina kujali iwapo yanakiuka makubaliano ya nyuklia ya Vienna au la.
Taarifa ya hivi karibuni ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ilibainisha kuwa: "Taasisi hii haiwezi kutekeleza jambo kwa mashinikizo ya kisiasa. Tuna taratibu mahususi za utendaji kazi."
Hii ni baada ya Nikki Haley, Balozi na mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, mwishoni mwa mwezi uliopita akiwa mjini Vienna alipokutana na Yukia Amano, Mkurugenzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kudai kuwa, mkataba huo wa JCPOA hautofautishi baina ya kukagua vituo vya kijeshi na visivyo vya kijeshi vya Iran.
Hii ni katika hali ambayo, Alkhamisi iliyopita, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) ulitoa ripoti yake mpya ukisisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza majukumu yake yote kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.