UNESCO: Watu Milioni 750 hawajui kusoma na kuandika duniani
(last modified Fri, 08 Sep 2017 07:43:24 GMT )
Sep 08, 2017 07:43 UTC
  • UNESCO: Watu Milioni 750 hawajui kusoma na kuandika duniani

Leo Septemba nane ni siku ya kimataifa ya kupinga ujinga wa kutojua kusoma na kuandika ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni 'kusoma na kuandika katika dunia ya kidijitali'.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO limesema, teknolojia za kidijitali zinapenya katika nyanja zote za maisha na kuathiri namna watu wanavyoishi, kujifunza na kushirikiana na jamii.

Licha ya kuweko fursa nyingi zinazojitokeza kutokana na teknolojia mpya na jinsi fursa hizo zinavyoimarisha maisha na kuwezesha watu kuja pamoja kimataifa, lakini kwa upande mwingine watu wasio na ujuzi wa kusoma na kuandika wanatengwa.

Kwa msingi huo, UNESCO inasema teknolojia inaweza kutumika kuimarisha ujuzi wa watu kujua kusoma na kuandika kwani hivi sasa kuna watu milioni 750 ambao ni wajinga wa kutojua kusoma na kuandika kote ulimwenguni.

Kama hiyo haitoshi, watoto na vijana milioni 264 hawanufaiki na elimu wanayopata shuleni.

Maosmo ya watu wazima

Katika ujumbe wake wa siku hii Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova amesema, ili kubuni na kuchukua fursa mpya kusongesha lengo namba nne la malengo ya maendeleo endelevu kuhusu elimu na mafunzo ya muda mrefu kwa wote, juhudi za pamoja zinahitajika ikiwemo ushirikiano  baina ya serikali, vyama vya umma na sekta binafsi kwa ajili ya kuimarisha ujuzi wa kusoma na kuandika.

Siku hii ambayo huadhimishwa kila mwaka inatoa fursa ya kutathmini hatua zilizopigwa na kuja pamoja, kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.