224 waaga dunia katika mtetemeko wa ardhi nchini Mexico
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34611-224_waaga_dunia_katika_mtetemeko_wa_ardhi_nchini_mexico
Kwa akali watu 224 wamepoteza maisha kutokana na mtetemeko mkubwa wa ardhi ulioikumba Mexico, ikiwa ni chini ya wiki mbili baada ya zilzala nyingine kuua makumi ya watu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 20, 2017 09:17 UTC
  • 224 waaga dunia katika mtetemeko wa ardhi nchini Mexico

Kwa akali watu 224 wamepoteza maisha kutokana na mtetemeko mkubwa wa ardhi ulioikumba Mexico, ikiwa ni chini ya wiki mbili baada ya zilzala nyingine kuua makumi ya watu nchini humo.

Zilzala hiyo iliyokuwa na ukubwa wa 7.1 kwa kipimo cha Rishta imeua watu 117 katika mji mkuu Mexico City na 98 kusini mwa nchi hiyo.

Miguel Osorio Chong, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico amesema mtetemeko huo umeua wanafunzi 21 baada ya paa la shule yao kuwaangukia viungani mwa Mexico City, huku 64 wakiripotiwa kupoteza maisha kutokana na janga hilo la kimaumbile katika jimbo la Morelos na 29 katika mji wa Puebla, kusini mashariki mwa mji mkuu huo.

Wananchi wakipekua vifusi kutafuta miili na manusuru Mexico

Mapema mwezi huu, mtetemeko mwingine mkubwa wa 8.1 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika pwani ya kusini ya Mexico yapata kilomita 120 kusini mashariki mwa mji mkuu Mexico City na kuua watu wasiopungua 90.

Tetemeko hilo la ardhi lilitajwa kuwa kubwa kabisa kuwahi kutokea nchini humo katika kipindi cha karne moja iliyopita.

Mwaka 1985 Mexico ilikumbwa na tetemeko la ardhi la ukubwa wa 8.0 kwa kipimo cha Rishta ambapo watu karibu elfu 10 waliaga dunia.