WHO yatahadharisha kuhusu hali iliyopo katika kambi za Waislamu wa Myanmar
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika kambi za wakimbizi huko Bangladesh unaotishia maisha ya Waislamu wa Rohingya wa Myanmar wapatao 436,000.
Shirika la Afya Duniani limetoa taarifa na kueleza kuwa milipuko ya magonjwa mbalimbali khususan kipindupindu katika kambi wanamoishi wakimbizi wa Rohingya huko Bangladesh inatia wasiwasi mkubwa kutokana na kushindwa raia hao kupata maji safi na salama pamoja na suhula za kitiba. Afisa mmoja wa Bangladesh amenukuliwa katika taarifa hiyo ya WHO akieleza kuwa wakimbizi Waislamu wa Rohingya karibu 4500 wameambukizwa kuhara katika muda wa mwezi mmoja uliopita.
Taarifa hiyo imeendelea kubainisha kuwa kambi hizo zinazowahifadhi Waislamu wa Rohingya ambazo sasa kwa haraka zimegeuka na kuwa kambi kubwa zaidi duniani zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na madawa na zinahitaji misaada mingi ya kibinadamu na ya haraka sana. Waislamu wa Rohingya wa Myanmar zaidi ya elfu sita wameuawa na wengine elfu nane kujeruhiwa hadi sasa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya ukandamizaji ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya jamii hiyo ya walio wachache katika mkoa wa Rakhine nchini humo tarehe 25 mwezi Agosti mwaka huu. Mkoa wa Rakhine unaopatikana magharibi mwa Myanmar tangu mwaka 2012 hadi sasa umekumbwa na mashambulizi ya jeshi la Myanmar na Mabudha wenye misimamo mikali wa nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa Rohingya.