WHO yaonya kuhusu unene miongoni mwa watoto duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35549-who_yaonya_kuhusu_unene_miongoni_mwa_watoto_duniani
Shirika la Afya Duniani, WHO, limeonya kuhusu idadi ya watoto na vijana barubaru walio na tatizo la unene au utipwatipwa duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 12, 2017 03:02 UTC
  •  WHO yaonya kuhusu unene miongoni mwa watoto duniani

Shirika la Afya Duniani, WHO, limeonya kuhusu idadi ya watoto na vijana barubaru walio na tatizo la unene au utipwatipwa duniani.

Katika taarifa WHO imesema idadi ya watoto na vijana barubaru wa kati ya umri wa miaka 5 hadi 19 walio na tatizo la unene imeongezeka kote duniani katika miongo minne iliyopita. Shirika hilo limeonya kuwa endapo hali ya sasa itaendelea basi watoto na barubaru wengi watakuwa na unene wa kupindukia.

Ripoti iliyochapishwa kwenye jarida la afya la Uingereza Lancet katika kuadhimisha Siku ya Unene Duniani, iliyoadhimishwa jana Oktoba 11, inasema kiwango cha utipwatipwa kimeongezeka kutoka chini ya asilimia moja 1975 na kufikia karibu asilimia 6 kwa wasichana sawa na milioni 50 na asilimia 8 kwa wavulana sawa na milioni 74 mwa 2016.

Kwa ujumla unene kati ya umri wa miaka 5-19 umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 10 duniani kutoka milioni 11 mwaka 1975 na kufikia milioni 124 2016.

Mgogoro wa unene duniani

Ili kukabiliana na tatizo hilo WHO imetoa mapendekezo sita ya kuzingatiwa kupambana na utipwatipwa zikiwemo  será za kudhibiti matangazo ya chakula na bei zinazochangia hali hii. Fiona Bull ni meneja mipango, ufuatiliaji na uzuiaji wa maradhi yasiyo ya kuambukiza wa WHO anasema kuna haja ya kuhakikisha mazingira ya shule yanaandaliwa ili watoto wetu wapate fursa ya chakula bora na mazoezi ya mwili.

Ameongeza kuwa bila kudhibitiwa utipwatipwa kuna hatari kubwa ya watoto na vijana kutumbukia katika maradhi yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo, kisukari, na saratani ambayo yana gharama kubwa kutibu kuliko kukinga.