Umoja wa Ulaya: Tutaiwekea vikwazo na mashinikizo zaidi Korea Kaskazini
Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ametangaza azma ya umoja huo ya kuzidisha vikwazo na mashinikizo zaidi ya kiuchumi dhidi ya Korea Kaskazini.
Bi Federica Mogherini ameyasema hayo baada ya kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje cha wanachama wa EU mjini Brussels, Ubelgiji na kuongeza: "Katika kikao tumejadili masuala mengi kukiwemo kupasishwa azimio dhidi ya Korea Kaskazini." Mwisho wa kunukuu.
Ameongeza kwa kusema kuwa, hatua mpya ya Umoja wa Ulaya dhidi ya Pyongyang inajumuisha marufuku ya kuizuia kikamilifu nchi hiyo ya Asia kufanya shughuli zozote ndani ya nchi wanachama wa EU. Kadhalika Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amezungumzia marufuku ya kuiuzia Korea Kaskazini mafuta yaliyosafishwa na mafuta ghafi. Aidha kuzuia kuongezewa vibali vya kuendesha shughuli ndani ya nchi za umoja huo kwa raia wa Korea Kaskazini na kadhalika kuwekewa mashinikizo asasi za nchi hiyo, ni miongoni mwa hatua nyingine zilizochukuliwa katika kikao hicho cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa EU. Federica Mogherini amesisitiza kuwa umoja huo utaendelea kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya Pyongyang kama ambavyo pia amezitaka taasisi mbalimbali duniani kufuata mkondo huo.
Mogherini amedai kuwa, lengo la hatua hizo ni kuisukuma nchi hiyo kuketi kwenye meza ya mazungumzo na kwamba kwa mujibu wa uzoefu, mashinikizo na vikwazo vya kiuchumi na kidemokrasia vinaweza kuandaa anga kwa ajili ya kufanyika mazungumzo ya kidiplomasia. Katika kulalamikia harakati za uhasama na kijeshi za Marekani na washirika wake dhidi ya Pyongyang, mwezi uliopita Korea Kaskazini ilifanyia jaribio la sita na lenye uwezo mkubwa la silaha ya nyuklia.