Oct 17, 2017 15:11 UTC
  • 71 wauawa katika mashambulizi ya kigaidi ya Taliban, Afghanistan

Watu wasiopungua 71 wameuawa huku wengine 200 wakijeruhiwa katika wimbi jipya la mashambulizi ya kigaidi ya kundi la Taliban nchini Afghanistan leo Jumanne.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo imesema, katika shambulizi la kwanza, gari lililokuwa limesheheni mada za milipuko liliripuka katika chuo cha mafunzo ya polisi katika mji wa Gardez, makao makuu ya mkoa wa Paktia, ambapo watu 32 wameuawa huku mamia ya wengine wakijeruhiwa.

Katika tukio jingine tofauti, magaidi hao wa Taliban wameshambulia kituo cha polisi na kituo cha upekuzi katika wilaya ya Andar mkoani Ghazni kusini mwa nchi, ambapo watu 15 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa.

Aidha maafisa watatu wa usalama wameuawa baada ya wachama wa genge hilo la kigaidi kushambulia ofisi ya serikali katika wilaya ya Shibkho, mkoani Farah, magharibi mwa nchi.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Taliban

Genge la kigaidi na kitakfiri la Taliban limetangaza kuhusika na wimbi hilo la mashambulizi ya kigaidi, huku likiapa kuendeleza hujuma hizo hadi pale vikosi vyote vya kigeni vitakapoondoka katika ardhi ya nchi hiyo.

Mashambulizi haya yanafanyika licha ya Rais Donald Trump wa Marekani hivi karibuni kuidhinisha kutumwa askari elfu nne zaidi nchini Afghanistan,  waliojumuishwa na wenzao 8,400 waliokuweko nchini humo; mbali wengine elfu tano wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO). 

Tags