Katibu Mkuu wa UN ataka mapambano ya kimataifa dhidi ya umaskini
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kuendeshwa mapambano ya kutokomeza vyanzo vya umaskini duniani.
Akizungumza jana katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini, Antonio Guterres ametuma ujumbe akisisiza umuhimu wa kuendeshwa mapambano dhidi ya umaskini duniani. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza katika ujumbe wake huo kuhusu kushiriki pande zote na kutafuta njia ya kuendeleza mapambano dhidi ya umaskini duniani.
Guterres ametaka pia kukabiliana na masuala yanayosababisha umaskini na vile vile ametaka kufanyika juhudi ili kuzisaidia jamii maskini katika maeneo mbalimbali duniani. Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini kwa lengo la kuhakikisha kuwa ulimwengu unakuwa salama na kunakuwepo jamii iliyo na amani ili kudhamini suhula za maisha kwa ajili ya wote imeafikiwa na jamii ya kimataifa.
Ripoti mbalimbali zilizotolewa zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu milioni 800 duniani wanaishi katika lindi kubwa la umaskini na wengine wengi wanakabiliwa na tishio la ajira, ukosefu wa amani, uadilifu, na pia athari za mabadiliko ya tabianchi. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1992 lilitangaza tarehe 17 mwezi Oktoba kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya kutokomeza umaskini.