Maelfu ya wananchi wa Korea Kusini waandamana dhidi ya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i36182-maelfu_ya_wananchi_wa_korea_kusini_waandamana_dhidi_ya_trump
Maelfu ya wananchi wa Korea Kusini wamefanya maandamano ya kukashifu kile wanachotaja kama chokochoko za Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ameanza safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za Asia, dhidi ya Korea Kaskazini.
(last modified 2026-02-02T06:45:47+00:00 )
Nov 05, 2017 14:47 UTC
  • Maelfu ya wananchi wa Korea Kusini waandamana dhidi ya Trump

Maelfu ya wananchi wa Korea Kusini wamefanya maandamano ya kukashifu kile wanachotaja kama chokochoko za Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ameanza safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za Asia, dhidi ya Korea Kaskazini.

Waandamanaji wapatao elfu tano wameripotiwa kushirika maandamano hayo ya jana Jumamosi, katika mji mkuu wa nchi hiyo Seoul, ambapo wamekashifu safari ya Trump nchini humo ndani ya siku chache zijazo, wakisema kuwa itazidisha taharuki katika Pensula ya Korea.

Waandamanaji hao kutoka makundi ya siasa za mrengo wa kushoto 220, asasi za kiraia, vyama vya wafanyakazi na miungano ya wanafunzi walikusanyika nje ya ubalozi wa Marekani mjini hapo, huku wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe za kumkashifu Trump ambaye anashinikiza kushambuliwa kijeshi Korea Kaskazini.

Rais Trump na Waziri Mkuu wa Japan

Baadhi ya mabango hayo yalikuwa yameandikwa "Hatumtaki Trump, Hatutaki vita", "Simamisha Vita".

Uhusiano kati ya Marekani na Korea Kusini uliingia doa katika miezi ya hivi karibuni, baada ya kutofautiana jinsi ya kukabili mgogoro wa nyuklia wa Korea Kaskazini.

Trump anazitembelea nchi tano za Asia ambazo ni Japan, Korea Kusini, China, Vietnam na Ufilipino. Trump na marais wenzake wa nchi za Japan na Korea Kusini wanatazamiwa kutuma ujumbe mzito kwa Pyongyang ili Korea Kaskazini itazame upya miradi yake ya makombora na silaha za nyuklia.