Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Tabianchi waanza Ujerumani
Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Tabianchi ulianza jana Jumatatu na utaendelea hadi tarehe 17 Novemba katika mji mwa Bonn nchini Ujerumani.
Kongamano hilo ambalo ni maarufu kama COP23 (Conference of Parties) na ni kikao cha nchi zilizotia saini mkataba wa kimataIfa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi wa Paris.
Mapatano ya Kwanza ya Kimataifa ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi yalitiwa saini na nchi 196 Desemba mwaka 2015 mjini Paris na Novemba mwaka 2016 mktaba huo ulianza kutekelezwa. Hadi sasa ni nchi 169 zilizoidhinishwa mkataba huo. Lengo la mkataba huo ni kuzuia ongezeko la joto duniani kwa nyuzi joto 2C.
Hivi sasa ni fursa kwa nchi za dunia kutathmini na kuchunguza hatua zilizochukuliwa na kutizama mustakabali katika utekelezwaji wa mkataba huo wa mabadiliko ya tabianchi. Katibu Mkuu mtendaji wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi UNFCCC Patricia Espinosa, anamini kuwa, muda wa kubadilisha hali ya mambo unakaribia kumalizika na kunapaswa kuwepo jitihada za haraka na za kina kwa ajili ya kupunguza uchafuzi wa mazingira ya dunia.
Inatarajiwa kuwa, kongamano la Bonn litagubikwa na uamuzi tata wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kuiondoa nchi yake katika mapatano ya tabianchi ya Paris. Trump, kinyume cha Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani ambaye alikuwa miongoni mwa waungaji mkono wa mapatano ya Paris, kwa mara kadhaa sasa ameukosoa vikali mkataba huo na kusema ni kizuizi katika kufikia malengo yake ya kuboresha uchumi wa Marekani hasa katika sekta za viwanda na nishati.
Trump anatoa misimamo ya kikaidi katika hali ambayo Marekani ni kati ya nchi zinazoongoza katika uchafuzi wa mazingira na hivyo kusababisha ongezeko la joto duniani kutokana na viwanda vyake. Hatua ya Trump ya kupinga mapatano ya Paris si tu kuwa imewakasirisha viongozi wa nchi ambazo zinaibuka upya kiuchumi bali hata Kansela Angela Merkel wa Ujerumani hivi karibuni katika kikao cha nchi tajiri kiviwanda maarufu kama G7 alitumia istilahi ya G6 akiashiria kuungana wanachama wengine wa kundi hilo dhidi ya Marekani. Merkel aidha alisisitiza kuwa kinyume na anavyotaka Trump, hakutafanyika mazungumzo mapya kuhusu mapatano ya tabianchi ya Paris.
Kwa kujiondoa Marekani katika mapatano ya Paris, kuna hatari kuwa nchi zingine ambazo pia zinachangia pakubwa katika uchafuzi wa mazingira nazo pia zitakiuka kwa njia moja au nyingine mapatano hayo ya Paris. Hilo ni jambo ambalo bila shaka litakuwa na madhara yasiyoweza kufidiwa na hatimaye kusababisha hasara kubwa kwa wakazi wa sayari ya dunia. Kwa mtazamo wa Trump, hakuna ukweli wowote katika kadhia ya kuongoezeka joto duniani na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa Andrei Belousov mshauri wa Rais wa Russia katika masuala ya mazingira, ni wazi kuwa, pasina kushiriki Marekani, mapatano ya Paris hayatakuwa na taathira kwani Marekani ndiye mzalishaji mkubwa zaidi wa gesi zinazochafua mazingira duniani.
Weledi wa mambo wanasema hata kama Marekani imetangaza kujiondoa katika mapatano ya Paris, itachukua miaka kadhaa kabla ya kuondoka rasmi katika mapatano hayo. Pamoja na hayo sayari ya dunia inaendelea kukabiliwa na hatari ya ongezeko la joto duniani kwa sababu Marekani ingali inaendelea kutekeleza sera zenye kuchafua mazingira ya dunia.
Hii ni katika hali ambayo, mwaka huu wa 2017 unatarajiwa kawa miongoni mwa miaka mitatu iliyovunja rekodi ya kuwa na jioto kali katika historia ya sayari ya dunia.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) iliyotolewa jana huku dunia ikiendelea kukumbwa na majanga makubwa kama vimbunga, mafuriko, mawimbi joto na ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi.