Korea Kaskazini: Trump mzee kichaa, lini ataanzisha vita vya nyuklia?
Gazeti la chama tawala nchini Korea Kaskazini la Roodong Simon limemtaja Rais Donald Trump wa Marekani kuwa ni 'mzee kichaa'.
Gazeti hilo pia limeandika kuwa, 'Hakuna mtu anayeweza kutabiri ni lini mzee huyo wa White House na aliyepoteza akili, ataanzisha vita vya nyuklia.' Gazeti la Roodong Simon sambamba na kumtaja Trump kuwa muhusika mkuu wa kushtadi mgogoro wa eneo la Korea limeandika kuwa, katika kujibu matamshi ya kipumbavu ya Trump aliyoyatoa katika safari yake nchini Japan, Pyongyang italipiza kisasi bila ya huruma. Itakumbukwa kuwa, katika safari yake mjini Tokyo, Japan Trump alisema kuwa, Marekani inaandaa mpango kwa ajili ya kukabiliana na hujuma hatari tarajiwa ya Korea Kaskazini.
Kabla ya hapo pia serikali ya Korea Kaskazini ilimtaja Rais Donald Trump kuwa aliye na matatizo ya kiakili. Katika mwendelezo wa safari yake barani Asia na akiwa nchini Korea Kusini hii leo Trump pia ametoa vitisho vingine kuilenga Pyongyang na kusema kuwa, Washington imejiandaa kutumia nguvu zake zote za kijeshi ikiwa italazimika kufanya hivyo ili kujilinda na kuwalinda marafiki zake wa eneo la Korea kutokana na hatari ya Korea Kaskazini. Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa Korea Kaskazini wameendelea kusisitiza umuhimu wa kujiimarisha kwa silaha za nyuklia baada ya vitisho vya Trump tangu alipoingia madarakani nchini Marekani.