Kuongezeka mivutano ya kisiasa kati ya Ujerumani na Saudia
Matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel dhidi ya utawala wa kifalme wa Saudi Arabia na majibu ya utawala huo vimezidisha mivutano kati ya nchi hizo mbili.
Sigmar Gabriel alitahadharisha Ijumaa iliyopita kwamba sera za vituko na hatari za utawala wa Saudi Arabia zinapanuka zaidi na kwamba Ulaya haitanyamaza kimya mbele ya mienendo hiyo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani pia ameashiria mashambulizi ya Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen na mgogoro wa Riyadh na washirika wake pamoja na Qatar na kusema: Mwenendo wa Saudia kuhusiana na Lebanon ni kilele cha mgogoro katika Mashariki ya Kati.
Mapema jana Jumamosi Saudi Arabia imemwita nyumbani balozi wake mjini Berlin ikilalamikia matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani. Taarifa ya Wizawa ya Mambo ya Nje ya Saudia imesema kuwa, matamshi hayo yameishangaza serikali ya Riyadh.
Inaonekana kuwa Berlin imeamua kutumia siasa za kindumakuwili kuhusiana na serikali ya Riyadh. Katika upande mmoja Ujerumani inashambulia vikali mienendo na sera za Saudi Arabia katika eneo la Mashariki ya Kati ikizitaja kuwa ni hatari. Matamshi haya ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani yanaakisi ukweli na hakika ya sera za utawala wa kifalme wa Saudi Arabia hususan baada ya kushika madaraka timu mpya inayoongozwa na Mfalme Salman na mwanaye Muhammad ambako kunashuhudiwa hujuma na mashambuklizi ya utawala huo dhidi ya nchi za eneo hilo. Mfano wa wazi wa sera hizo za hujuma na vita ni mashambulizi ya Saudia dhidi ya watu wa Yemen yaliyoanza Machi mwaka 2015 na hadi sasa yameua maelfu ya raia wasio na hatia hususan wanawake na watoto wadogo.
Katika upande mwingine baada ya kushindwa mtawalia huko Syria kutokana na kushindwa mara kwa mara makundi ya kigaidi yanayosaidiwa kwa hali na mali ya serikali ya Riyadh, utawala wa Saudia unapanga mikakati ya kuanzisha machafuko mengine huko Lebanon na ili kufikia lengo hilo inatumia suala la kujiuzulu kwa kwa kulazimishwa Waziri Mkuu wa Lebanon, Saad al Hariri na kuzidisha mashinikizo dhidi ya harakati ya Hizbullah. Harakati hizo za Saudia zimekabiliwa na upinzani mkubwa wa Lebano, nchi za Mashariki ya Kati na hata waitifaki wa Kimagharibi wa serikali ya Riyadh. Msimamo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani dhidi ya Saudia yanaweza kutathminiwa katika mkondo huo.
Hata hivyo kunajitokeza swali kwamba, je, tunapaswa kuamini ukosoaji mkali wa Ujerumani dhidi ya Saudi Arabia au tuamini hali halisi inayotawala uhusiano wa nchi hizo?
Ripoti iliyotolewa hivi karibuni inasema kuwa, mauzo ya silaha za Ujerumani kwa Saudi Arabia yameongeka karibu mara nne, na Wasaudia wanatumia silaha hizo kuua raia wa Yemen. Hivyo basi, kama kweli Berlin inapinga sera na siasa za kupenda vita na kuhatarisha amani za Saudia, kwa nini inaendeleza uhusiano wa karibu na utawala huo wa kifalme sambamba na kuzidisha mara nne mauzo ya silaha zake kwa utawala huo?
Katika uwanja huo mwakilishi wa chama cha kushoto nchini Ujerumani, Stephen Leibish anasema: "Mauzo ya silaha ya serikali ya Ujerumani kwa Saudia ni hatua ya kuaibisha", mwisho wa kunukuu. Inasikitisha sana kuona kwamba, katika miaka ya hivi karibuni Ujerumaji imedumisha na kupanua zaidi uhusiano wake wa kijeshi na wa masuala ya silaha na utawala wa Saudi Arabia licha ya kutambua faili jeusi la utawala huo kuhusu haki za binadamu ndani na nje ya nchi hiyo. Ni vyema pia tukumbushe hapa kuwa, Berlin ni miongoni mwa washirika wakuu wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia katika masuala ya mauzo ya silaha na kutoa mafunzo ya kijeshi kwa askari wa utawala huo.
Agnieszka Brugger ambaye ni mwanasiasa na mtaalamu wa masuala ya ulinzi wa chama cha Green nchini Ujerumani ameashiria ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na Saudi Arabia na kusisitiza kuwa, Ujerumani inapaswa kusitisha mikataba yote ya mauzo ya silaha kwa nchi kama Saudi Arabia.
Ukweli ni kwamba japokuwa yaliyosemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani kuhusu Saudi Arabia yaanakisi haki na kweli lakini tunapaswa kutambua kuwa, Berlin imechukua siasa za kinafiki na kidhabadhabina kuhusiana na Riyadh. Suala hili linaonesha kuwa, jambo lenye umuhimu kwa Wamagharibi ikiwemo Ujerumani, ni maslahi ya kifedha na kiuchumi na si haki za binadamu.