EU yaipa Uingereza siku 10 kuamua kuhusu kujitoa katika umoja huo
-
Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza
Donald Tusk, mkuu wa Baraza la Umoja wa Ulaya ameipa Uingereza muda wa siku 10 kuhakikisha kunapatikana maendeleo ya kuridhisha katika mjadala wa kujitoa nchi hiyo kwenye Umoja wa Ulaya.
Mapema leo asubuhi, shirika la habari la IRNA limeunukuu Umoja wa Ulaya ukimpa siku kumi waziri mkuu wa Uingereza, Theresa May, ili kuandaa mazingira ya kujitoa katika umoja huo na kuwashawishi wakuu wa Umoja wa Ulaya kuanzisha mazungumzo ya kibiashara katika kikao chao cha mwezi Disemba.
Baada ya kuonana na Theresa May, huko Brussels, Ubelgiji, Donald Tusk, mkuu wa Baraza la Umoja wa Ulaya amesema kuwa, inabidi katika kipindi cha siku kumi zijazo, Uingereza ipige hatua nzuri katika masuala yote ikiwa ni pamoja na suala la kuanisha mpaka wake na Ireland.
Amesema, iwapo hadi kufikia mwezi ujao wa Disemba hakutakuwa kumefikiwa maendeleo yoyote katika mazungumzo ya Umoja wa Ulaya na Uingereza, basi mashinikizo yataongezeka kwa Waingereza na wafanyabiashara wake watapata hasara.
Inatarajiwa kuwa siku ya Jumatatu ya tarehe 4 Disemba, Theresa May ataonana na Jean-Claude Juncker, mkuu wa Kamisheni ya Ulaya kuzungumzia suala la kujitoa Uingereza katika umoja huo.
Uingereza inatarajiwa kumaliza mchakato wa kujitoa kikamilifu katika Umoja wa Ulaya ifikapo mwezi Machi mwaka 2019.