Korea Kaskazini yavurumisha kombora la balestiki kuelekea Japan
Korea Kaskazini imefyatua kombora jengine la balestiki lililopaa juu ya kisiwa cha Japan na linaloweza kulenga sehemu yoyote ya ardhi ya Marekani, huku ikisisitiza kuwa sasa ina uwezo kamili wa kinyuklia.
Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini (KCNA) limesema kombora hilo jipya la balestiki lililofanyiwa majaribio na Pyongyang na linalofahamika kama Hwasong-15, liliruka angani kwa takriban dakika 53 hivi kabla ya kudondoka katika kisiwa cha Japan.
KCNA imesema kombora hilo jipya la ICBM limeruka angani umbali wa kilomita 4,475, umbali wa juu kabisa wa makombora yote yaliyovurumishwa na Pyongyang huko nyuma.
Baada ya kushuhudia jaribio hilo, kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un ametangaza kuwa nchi hiyo sasa ina uwezo kamili wa kinyuklia na inajifakharisha kufikia hatua hiyo. Katika taarifa, Kim Jong-un amesema kombora hilo la balestiki lina uwezo wa kulenga kona yoyote ile ya ardhi ya Marekani.
Hatua hiyo hiyo ya Pyongyang hata hivyo imekosolewa vikali na duru mbalimbali za kimataifa, akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres; huku Marekani, Japan na Korea Kusini zikitoa wito wa kufanyika mkutano wa dharura hii leo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili kadhia hiyo.