Kushadidi hatua za chuki za Trump dhidi ya Uislamu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i37011-kushadidi_hatua_za_chuki_za_trump_dhidi_ya_uislamu
Kitendo cha Rais Donald Trump wa Marekani cha kusambaza tena filamu za vidio za propaganda za chuki dhidi ya Uislamu kupitia ukurasa wake wa Twitter kimezusha moto wa ghadhabu na hasira duniani. Hatua hiyo ya Trump ya kuweka tena filamu hizo za vidio za kuchochea chuki dhidi ya Uislamu imelaaniwa kuanzia ndani ya Marekani na wapinzani wake mpaka na viongozi wa nchi nyengine duniani.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Nov 30, 2017 23:16 UTC
  • Kushadidi hatua za chuki za Trump dhidi ya Uislamu

Kitendo cha Rais Donald Trump wa Marekani cha kusambaza tena filamu za vidio za propaganda za chuki dhidi ya Uislamu kupitia ukurasa wake wa Twitter kimezusha moto wa ghadhabu na hasira duniani. Hatua hiyo ya Trump ya kuweka tena filamu hizo za vidio za kuchochea chuki dhidi ya Uislamu imelaaniwa kuanzia ndani ya Marekani na wapinzani wake mpaka na viongozi wa nchi nyengine duniani.

Siku ya Jumatano, Rais huyo wa Marekani aliziweka tena kwenye ukurasa wake wa Twitter filamu za vidio zilizosambazwa na Jayda Fransen, naibu kiongozi wa kundi la mrengo wa kulia lenye misimamo ya kufurutu mpaka nchini Uingereza liitwalo "Uingereza Kwanza". Trump, ambaye ana wafuasi zaidi ya milioni 44 katika mitandao ya kijamii wanaofuatilia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, amedhihirisha kwa mara nyengine tena chuki zake dhidi ya Uislamu kwa kuzisambaza tena filamu hizo za vidio katika upeo mkubwa sana duniani.

Jayda Fransen

Bila ya shaka chuki za Trump kwa Uislamu si jambo jipya na geni. Mnamo mwaka 2015, na kabla ya kujitosa kwenye kampeni za kuwania urais wa Marekani, alidai kuwa "Uislamu unaichukia Marekani". Wakati wa kampeni za uchaguzi Trump aliahidi kuwa endapo atashinda na kuingia Ikulu ya White House atawazuia Waislamu wasiingie nchini Marekani. Kama vile haitoshi, katika hotuba yake ya mwanzo aliyotoa baada ya kutawazwa kuwa rais wa Marekani, Donald Trump alitumia kwa mara ya kwanza msamiati wa "Magaidi wa Kiislamu"; na wiki moja tu baada ya kukalia kiti cha urais akasaini amri ya kuwapiga marufuku raia wa nchi saba za Waislamu wasiingie nchini Marekani.

Trump akisaini dikrii ya kupiga marufuku raia wa mataifa saba ya Waislamu wasiingie Marekani

Pamoja na hayo, hakuna yoyote kati ya matamshi na hatua alizochukua huko nyuma Trump ambazo zimedhihirisha na kuweka wazi zaidi msimamo wa rais huyo wa Marekani wa kuwa kitu kimoja na harakati za ubaguzi wa rangi na za chuki dhidi ya Uislamu kama kitendo chake cha siku ya Jumatano cha kuweka kwenye ukurasa wake wa kijamii filamu tatu za vidio za muingereza mbaguzi wa rangi na mwenye misimamo ya kufurutu ada zinazoeneza chuki dhidi ya Uislamu. Hatua hiyo ya Trump imezusha wasiwasi na taharuki kiasi kwamba hata Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza, nchi ambayo ina uhusiano maalumu wa kistratijia na Marekani amekosoa vikali kitendo hicho kilichofanywa na rais wa nchi hiyo. Kufuatia ukosoaji huo, Trump ametumia lugha isiyo ya murua katika uhusiano wa London na Washington kwa kumshauri Bi Theresa May kwamba badala ya kumkosoa rais wa Marekani ashughulikie jukumu lake la kupambana na magaidi.

Kuna ushahidi kadhaa unaoonyesha kuwa Trump anajaribu kwa makusudi kuyafufua na kuyapa nguvu makundi ya kibaguzi na yenye misimamo ya kufurutu mpaka ndani na nje ya Marekani. Kwa rais wa sasa wa Marekani, hakuna tofauti yoyote kuwaunga mkono wazungu wabaguzi wa rangi walioonyesha chuki dhidi ya wamarekani weusi katika vurumai na machafuko ya kibaguzi yaliyotokea katika mji wa Charlottesville kwenye jimbo la Virginia, au kutoa msukumo na kuwa kitu kimoja na makundi ya ubaguzi wa rangi yenye chuki na Uislamu ya nchini Uingereza. Kwake yeye Trump, mtu, kundi au jamii yoyote ambayo asili ya utambulisho wake si ya madhehebu ya Uprotestanti wa Wazungu wa Kianglo-Saxon (WASP), inahesabika kwake kuwa si katika yeye na inapasa kutokomezwa.

Maandamano ya kulaani sera za kibaguzi za rais wa Marekani

Bernie Sanders, Seneta wa jimbo la Vermont kwa tiketi ya chama cha Democrat ameeleza kupitia taarifa aliyotoa kuhusu kitendo cha Trump cha kueneza filamu za vidio za chuki dhidi ya Waislamu kwamba: Trump anaeneza hofu na chuki dhidi ya Waislamu.

Kwa hakika tuna kila sababu ya kusema kwamba uenezaji fikra hiyo utakuwa mwanzo wa vita katika siku za usoni vitakavyotokana na asili, dini na ustaarabu wa watu; vinginevyo walimwengu wote wapaze sauti zao kwa pamoja kulaani mwenendo wa kueneza chuki wa Donald Trump na harakati ya ubaguzi wa rangi wa utaifa inayomuunga mkono rais huyo wa Marekani.../