Dec 09, 2017 07:33 UTC
  • Erdogan ataka Waislamu walio wachache Ugiriki waheshimwe

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ametoa mwito wa kuheshimwa haki za jamii ya Waislamu walio wachache nchini Ugiriki.

Erdogan alitoa wito huo hapo jana baada ya kushiriki Swala ya Ijumaa katika mji wa Komotini ulioko eneo la Thrace, kaskazini mashariki mwa Ugiriki.

Erdogan alipokelewa na umati mkubwa wa Waislamu wenye asili ya Uturuki ambao amewataja kama daraja kati ya Uturuki na Ugiriki, huku akisisitiza haja ya kudumishwa mshikamano na umoja.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, kuna takriban Waislamu wanaozungumza Kituruki laki moja na 50 elfu nchini Ugiriki.

Kabla ya hapo, Rais wa Uturuki katika mazungumzo yake na Alexis Tsipras, Waziri Mkuu wa Ugiriki alikosoa vikali kile alichokitaja kama 'ubaguzi' dhidi ya Waislamu, ambao ni katika jamii za wachache nchini humo, na kutaka haki zao ziheshimiwe kwa mujibu wa Mkataba wa Lausanne wa Mwaka 1923.

Wanawake Waislamu barani Ulaya

Mkataba huo ambao Ugiriki uliusaini, unasisitiza udharura wa kuheshimiwa haki za jamii za wachache, baada ya kusambaratika Utawala wa Othmaniyyah.

Ifahamike kuwa, Ugiriki kama zilivyo nchi nyingine za Ulaya inakabiliwa na wimbi la chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Mwishoni mwa mwaka uliopita, watu wenye chuki dhidi ya dini ya Kiislamu walipora na kuikalia kwa mabavu ardhi iliyokuwa imetolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa msikiti, katika mji mkuu Athens.

Tags