7 wakamatwa Italia kwa magendo ya wanawake wa Nigeria
Polisi nchini Italia imewatia mbaroni watu saba wanaotuhumiwa kuhusika na magendo ya wanawake wa Nigeria kwa ajili ya kuwaingiza katika biashara haramu ya ukahaba katika nchi hiyo ya Ulaya.
Kitengo maalumu cha polisi ya Italia kiitwacho Carabinieri kimesema waliokamatwa ni raia sita wa Nigeria na Muitaliano mmoja, na kwamba wanakabiliwa na mashitaka ya kufanya magendo ya binadamu, utumwa mamboleo, kuwafanya wanawake hao kuwa wahajiri kinyume cha sheria na kuwalazimisha kuingia katika ufuska.
Polisi ya Italia imesema imekuwa ikiendesha uchunguzi wa kina kwa karibu mwaka mmoja kwa shabaha ya kuvunja mtandao wa magendo ya binadamu katika nchi hiyo, Libya na Nigeria.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Wahajiri IOM, kumeshuhudia ongezeko la asilimia 600 ya magendo ya wanawake hususan wa Kinigeria wanaopelekwa Italia kwa ajili ya biashara ya ukahaba katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zilikutana katika kikao cha dharura na kusisitizia haja ya kuweko mapambano dhidi ya magendo ya binadamu na kung'olewa mizizi ya biashara ya utumwa barani Afrika.