Kuanza vita dhidi ya mitandao ya kijamii barani Ulaya
Kuanzia mwaka huu wa 2018 serikali ya Ujerumani inaanza kutekeleza sheria ambayo kwa mujibu wake mitandao ya kijamii yenye zaidi ya watumiaji milioni mbili italazimika kufuta posti na jumbe za mitandao ya kijamii zenye masuala yanayokiuka sheria hadi kufikia masaa 24 baada ya kupata habari za kuwepo jumbe kama hizo.
Makampuni ambayo hayataheshimu sheria hiyo yatakabiliwa na adhabu kali ya kutozwa faini ya kufikia Euro milioni 50.
Sheria hiyo katika daraja ya kwanza itaanza kutekelezwa kuhusu mitandao ya Tweeter, YouTube na Facebook. Utekelezaji wa sheria hiyo nchini Ujerumani ambayo ndiyo nchi muhimu zaidi katika Umoja wa Ulaya, utakuwa utangulizi wa kutekelezwa sheria kama hiyo katika nchi nyingine za Ulaya. Mbali na wahalifu wanaotumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya utapeli na udanganyifu, wizi wa mtandaoni, magendo ya binadamu, biashara haramu na kadhalika, nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani pia zina wasiwasi mkubwa kuhusu jinsi makundi ya kigaidi yanavyotumia mitandao hiyo ya kijamii. Rob Wainwright, Mkuu wa Polisi ya Ulaya (Europol) anasema: Kundi la Daesh linapanua vyombo vyake vya mawasiliano ya kijamii ili liweze kusambaza misimamo na harakati zake katika maeneo mbalimbali ya duniani." Lengo la kwanza la hatua kama hizi ni kusambaza na kuhalalisha misimamo ya kundi hilo la Daesh na lengo kuu muhimu zaidi ni kuwashawishi vijana wa Ulaya hususan wahajiri wa Kiislamu katika nchi kama Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kujiunga na kundi hilo na baadaye kutumiwa katika mashambulizi ya kigaidi barani humo.
Kutokana na ukubwa, ugumu na mbinu zinazotumiwa katika mitandao ya intaneti hususan mitandao ya kijamii, kundi la kigaidi la Daesh limeweza kupanua harakati na mashambulizi yake katika wavuti kupitia kwa wafuasi na wanachama wake.
Waziri wa Usalama wa Taifa wa Uingereza, Ben Wallace ameyakosoa makampuni ya mitandao ya kijamii kama Facebook, google na Youtube kutokana na kutoshirikiana na mamlaka za serikali na kuyataja kuwa ni makampuni yasiyo na huruma. Anasema makampuni hayo hayasaidii jitihada za kupambana na ugaidi na misimamo mikali licha ya kusambaa zaidi jumbe mbaya kupitia mitandao hiyo.
Mwezi Mei mwaka 2017 Polisi ya Ulaya (Europol) ilitangaza habari ya kupanuka zaidi mitandao ya kijamii ya makundi ya kigaidi barani humo na kusema kuwa, imegundua zaidi ya matangazo elfu mbili yenye uhusiano na harakatri za kundi la kigaidi la Daesh.
Kwa kutilia maanani hayo yote, inaoneka kuwa hatua ya serikali ya Ujerumani imechukuliwa kwa shabaha ya kukabiliana na mwenendo huo haribifu wa utumiaji mbaya wa mitandao ya kijamii kwa malengo haramu ya kiuchumi au mashambulizi ya kigaidi. Hata hivyo suala muhimu sana katika mapambano haya ni kiwango cha ushirikianao wa makampuni yanayomiliki mitandao. Pamoja na hayo misimamo ya kindumakuwili ya nchi za Ulaya na Magharibi kwa ujumla katika kukabiliana na mitandao ya kijamii na kuweka sheria kali kwa ajili ya mitandao hiyo huku nchi hizo hizo za Magharibi zikikosoa sheria kama hizo hizo zilizowekwa katika nchi nyingine dhidi ya mitandao hiyo, ni kielelezo cha sera na siasa zinazogongana za nchi hizo za Ulaya na Marekani.