Kuanza mazungumzo kati ya Korea mbili na kufikiwa makubaliano
https://parstoday.ir/sw/news/world-i38771-kuanza_mazungumzo_kati_ya_korea_mbili_na_kufikiwa_makubaliano
Baada ya kuwasili wawakilishi wa nchi mbili za Korea Kusini na Korea Kaskazini katika kijiji cha Panmunjom maarufu kwa jina la 'kijiji cha usitishaji vita' na kilichopo katika mpaka wa mataifa hayo mawili, hatimaye mazungumzo rasmi kati ya pande mbili hizo yalianza asubuhi ya jana Jumanne.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Jan 10, 2018 12:38 UTC
  • Kuanza mazungumzo kati ya Korea mbili na kufikiwa makubaliano

Baada ya kuwasili wawakilishi wa nchi mbili za Korea Kusini na Korea Kaskazini katika kijiji cha Panmunjom maarufu kwa jina la 'kijiji cha usitishaji vita' na kilichopo katika mpaka wa mataifa hayo mawili, hatimaye mazungumzo rasmi kati ya pande mbili hizo yalianza asubuhi ya jana Jumanne.

Hii ni mara ya kwanza baada ya karibu miaka miwili ambapo jumbe za Korea mbili zinakutana na kujadili masuala kadhaa muhimu. Kwanza ni juu ya michuano ya Olimpiki ya msimu wa baridi ambayo itafanyika nchini Korea Kusini mwezi Fubruari na uamuzi wa Korea Kaskazini wa kutuma timu ya wanamichezo wake kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo, suala ambalo kwa hakika limezifungulia pande mbili fursa ya kukutana jumbe za kisiasa za mataifa hayo hasimu. Pili ni kwamba Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini amefufua kwa mara nyingine tena siasa zilizokuwa zikitekelezwa na Kim Dae-jung, rais wa zamani wa nchi hiyo kati ya miaka 1998-2008, ambapo katika kipindi chake kulifikiwa makubaliano mazuri kati ya Seoul na Pyongyang.

Park Geun-hye, Rais wa zamani wa Korea Kusini aliyechochea uhasama

Kati ya makubaliano hayo ilikuwa ni kuanzishwa kijiji cha viwanda cha Kaesong na kukutana familia zilizotenganishwa kutoka pande mbili, suala ambalo lilisaidia pia kupunguza mivutano kati yao. Hata hivyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na kutokana na siasa za rais wa zamani wa Korea Kusini, Park Geun-hye zilizojengeka juu ya kufungamana na Marekani na kuzidisha mashinikizo ya kisiasa na kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini, si tu kwamba zilipelekea kusambaratisha anga hiyo iliyopatikana ya maelewano, bali zilichochea zaidi mgogoro wa kijeshi kati ya nchi hizo.

Moon Jae-in, rais wa sasa wa Korea Kusni anayetaka utatuzi wa mgogoro uliopo

Katika hali hiyo weledi wa mambo wametoa indhari kuhusiana na taathira hasi ya mwenendo huo. Alexey Maslov, mkuu wa kituo cha uchunguzi wa kistratijia nchini China kinachojishughulisha na masuala ya Asia ambaye pia ni raia wa Russia amesema: "Hali katika eneo la Peninsula ya Korea imekuwa mbaya sana na ikiwa kutatokea mapigano ambayo yataanzishwa na Marekani dhidi ya Korea Kaskazini na kadhalika jibu kali la Pyongyang kwa hujuma hiyo ambalo litaenda sambamba na kuzishambulia Korea Kusini na Japan, ni jambo ambalo litakuwa na taathira angamizi kwa eneo hilo." Mwisho wa kunukuu. Hata hivyo pamoja na Washington kuonyesha kufurahishwa na hatua ya kuanza mazungumzo hayo ya jana kati ya pande mbili, lakini kiukweli haitaki kuona mgogoro wa eneo hilo unapatiwa ufumbuzi.

Kiongozi wa Korea Kaskazini

Hii ni kwa kuwa kupatikana usalama katika eneo la Peninsula ya Korea, kutapelekea kukosekana kisingizio cha kuendelea kuwepo askari wa Marekani katika eneo tajwa. Pamoja na hayo Korea Kusini ambayo inahisi kukabiliwa na tishio kubwa, imekuwa ikifanya juhudi za kupatiwa ufumbuzi wa kisiasa mzozo huo. Katika uwanja huo, Kim Seung-ho, balozi wa Korea Kusini mjini Tehran amesema: "Mgogoro uliopo katika eneo la Korea umedumu kwa zaidi ya miaka 60 na tumeendelea kuishi katika anga hiyo. Hata hivyo tumefanikiwa kupunguza mvutano katika ngazi maalumu kiasi cha kuzuia kujiri kwa mapigno huku tukitumia pia udiplomasia. Hii ni kwa kuwa udiplomasia umekuwa ndio dira ya mwelekeo wa Korea Kusini na utaendelea kusalia hivyo." Mwisho wa kunukuu. Alaa kulli hal, duru mpya ya mazungumzo ya pande mbili imeandaa fursa kwa Seoul na Pyongyang kudhamini maslahi yao ya kitaifa na umuhimu wa kudumishwa usalama na amani katika eneo, sambamba na kuzuia mapigano na kupunguza mvutano kupitia makubaliano chanya baina yao.