CARE: Watu milioni 70 duniani wanakabiliwa na migogoro iliyotelekezwa
Shirika la kimataifa la misaada ya kibinadamu la CARE International limesema zaidi ya watu milioni 70 wamenasa katika migogoro iliyotelezwa na kupuuzwa kote duniani.
Ripoti iliyotolewa na shirika hilo jana Jumatatu inasema kuwa, mbali na Korea Kaskazini, mamilioni ya watu wanakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu katika nchi za Eritrea na Burundi.
Laurie Lee, Kaimu Katibu Mkuu wa CARE amesema watu milioni 70 wanapitia kipindi kigumu mbele ya upuuzaji wa asasi za kimataifa, huku akieleza masikitiko yake kuhusu namna baadhi ya migogoro imefumbiwa macho na nyingine kupewa uzito.
Ripoti hiyo ya CARE imepewa anwani inayosema: Kuteseka kimya kimya, migogoro 10 ya kibinadamu ambayo haikuangaziwa ipasavyo mwaka 2017.
Nchi 7 kati ya 10 zilizotajwa kwenye ripoti hiyo ni za bara Afrika. Mbali na Korea Kaskazini, Eritrea na Burundi, nchi nyingine ambazo mamilioni ya raia wake wanakabiliwa na migogoro ya kibinadamu kimya kimya ni Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasa ya Kongo, Mali, Vietnam, eneo la Ziwa Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Peru.