Wabunge wa Marekani wamtaka Trump aendelee kuipatia misaada UNRWA
Wawakilishi 102 wa chama cha Democrat nchini Marekani wamemuandikia barua Rais wa nchi hiyo wakimtaka asikate misaada ya kifedha kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).
Gazeti la Kizayuni la The Times of Israel limeandika kuwa katika barua yao hiyo kwa Rais Donald Trump, wabunge hao wa chama cha Democrat wameeleza kuwa kitendo cha kuikatia UNRWA misaada ya kifedha kina madhara kwa maslahi ya Marekani katika eneo hili.
Barua hiyo imeendelea kubainisha kuwa, hatua ya kusitisha misaada ya mamilioni ya dola ya Marekani kwa shirika la UNRWA itapelekea kushtadi hisia dhidi ya Israel na kupunguza matarajio ya kupatikana njia ya ufumbuzi inayotakiwa na Marekani katika mwenendo wa mapatano kati ya utawala wa Kizayuni na Wapalestina.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalotoa Misaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) liliasisiwa mwezi Disemba mwaka 1949 kwa mujibu wa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lengo likiwa ni kuwahudumia na kutoa misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina. Shirika hilo linawahudumiwa wakimbizi wa Kipalestina karibu milioni tano walioko Jordan, Syria, Lebanon na katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na vile vile katika Ukanda wa Ghaza.
Itakumbukwa kuwa mwezi Januari mwaka huu Rais wa Marekani alisimamisha kulipatia shirika la UNRWA msaada wa dola milioni 65 ikiwa ni katika muendelezo wa hatua za chuki na uhasama kwa wananchi waliodhulumika wa Palestina.