Korea Kaskazini ilikataa kukutana kwa siri na viongozi wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i40671-korea_kaskazini_ilikataa_kukutana_kwa_siri_na_viongozi_wa_marekani
Imebainika kuwa, viongozi wa Korea Kaskazini walifuta ghafla mkutano wa faragha uliotatarajiwa kufanyika kati yao na Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence huko nchini Korea Kusini.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Feb 21, 2018 04:20 UTC
  • Korea Kaskazini ilikataa kukutana kwa siri na viongozi wa Marekani

Imebainika kuwa, viongozi wa Korea Kaskazini walifuta ghafla mkutano wa faragha uliotatarajiwa kufanyika kati yao na Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence huko nchini Korea Kusini.

Ofisi ya Mike Pence imeliambia gazeti la The Washington Post kuwa, Makamu wa Rais wa Marekani alitazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo ya siri mnamo Februari 10 mjini Pyeongchang nchini Korea Kusini na Kim Yo-jong, dada mdogo wa Kim Jong-un, kiongozi wa Korea Kaskazini na Kim Yong-nam, rais asiye na mamlaka kamili wa Korea Kaskazini, lakini viongozi wa Pyongyanga wakafuta mkutano huo katika dakika za mwisho.

Habari zinasema kuwa, Pyongyang ilifutilia mbali mkutano huo masaa mawili kabla uanze, baada ya Pence akiwa katika safari yake ya kiduru barani Asia kukosoa vikali uongozi wa Korea Kaskazini na kutaka Pyongyang iwekewe vikwazo vikali zaidi.   

Marekani na Korea Kaskazini zimekuwa zikitunishiana misuli

Itakumbukwa kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini mapema mwezi huu ilisisitiza kuwa, viongozi wa nchi hiyo ambao walipangiwa  kufanya safari nchini Korea Kusini kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi mjini Pyeongchang, kamwe hawangekutana na viongozi wa Marekani.

Marekani inatajwa kuwa chanzo cha kushtadi mzozo kati ya Korea mbili hasa kutokana na hatua za Washington kufanya maneva mtawalia ya kijeshi katika Rasi ya Korea sambamba na matamshi ya vitisho ya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya nchi hiyo.