Mar 12, 2018 02:30 UTC
  • Maadui watangaza

Taharuki imetanda miongoni mwa Waislamu nchini Uingereza baada ya kundi lenye chuki dhidi ya Uislamu kusambaza barua za kutaka kushambuliwa Waislamu na misikiti nchini humo.

Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar, Waingereza katika mji wa London na maeneo ya West Midlands na Yorkshire wamesema wamepokea barua hizo, zinazowataka kufanya hujuma dhidi ya Waislamu na maeneo yao ya ibada mnamo Aprili 3, siku ambayo wameiita 'Siku ya Kumwadhibu Muislamu'.

Sehemu moja ya barua hiyo imetangaza zawadi ya alama 10 kwa kumshambuliwa kwa matusi Muislamu, alama 50 kwa yule atayemwagia tindikali Muislamu, pointi elfu moja kwa atakayeshambulia msikiti, na alama 2,500 kwa yule atakayeishambulia kwa silaha za atomiki nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu al Kaaba huko Makka, Saudi Arabia.

Miqdaad Versi, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Uingereza amelaani vikali kusambazwa barua hizo zinazoashiria kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, lakini pia amebainisha kuwa kitendo hicho kimewaweka Waislamu wa nchini Uingereza katika hali ngumu, huku akiitaka polisi kuchunguza tukio hilo na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wahusika wake.

Msikiti mjini London, UK

Takwimu zinaonyesha kuwa, uhalifu unaotokana na chuki dhidi ya Waislamu na hujuma dhidi ya misikiti nchini Uingereza uliongezeka maradufu katika mwaka uliopita wa 2017 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake. 

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Jeremy Corbyn, kiongozi wa chama cha Leba cha nchini Uingereza alisema kuwa, chuki dhidi ya Uislamu ni tatizo kwa jamii ya nchi hiyo ya barani Ulaya licha ya kwamba dini ya Uislamu ni nembo ya amani na kujitolea.

Kuna zaidi ya Waislamu milioni 2 na laki 5 huko Uingereza, na Uislamu unahesabiwa kuwa dini ya pili yenye idadi kubwa ya wafuasi nchini humo.

Tags