Kupigwa kalamu nyekundu Tillerson; mtingishiko ndani ya serikali ya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i41643-kupigwa_kalamu_nyekundu_tillerson_mtingishiko_ndani_ya_serikali_ya_trump
Hatimaye Rex Tillerson amepigwa kalamu nyekundu na kuuzuliwa wadhifa wa uwaziri wa mambo ya nje wa Marekani. Rais Donald Trump wa Marekani ametoa ujumbe kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter wa kutangaza moja ya mabadiliko makubwa ya baraza la mawaziri katika kipindi cha urais wake.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Mar 14, 2018 04:50 UTC
  • Kupigwa kalamu nyekundu Tillerson; mtingishiko ndani ya serikali ya Trump

Hatimaye Rex Tillerson amepigwa kalamu nyekundu na kuuzuliwa wadhifa wa uwaziri wa mambo ya nje wa Marekani. Rais Donald Trump wa Marekani ametoa ujumbe kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter wa kutangaza moja ya mabadiliko makubwa ya baraza la mawaziri katika kipindi cha urais wake.

Katika ujumbe wake huo Trump ameandika: "Mike Pompeo, Mkurugenzi wa CIA atakuwa waziri mpya wa mambo ya nje. Yeye ataifanya vizuri sana kazi hii! Namshukuru Rex Tillerson kwa utumishi wake! Gina Haspel atakuwa Mkurugenzi mpya wa CIA na mwanamke wa kwanza kuchaguliwa katika cheo hiki. Hongera kwa wote!"

Kwa ujumbe huo wa twitter hatima ya nyadhifa mbili muhimu katika serikali ya Trump imejulikana. Mike Pompeo ni mmoja wa viongozi waaminifu zaidi kwa serikali ya Trump ambaye ametoka shirika la ujasusi la nchi hiyo CIA na kuhamishiwa wizara ya mambo ya nje ili kupoza joto la moto wa upinzani na mvutano linalozidi kutokota kwenye jungu la chombo hicho kikuu cha diplomasia cha Marekani kati ya aliyekuwa nahodha wake Rex Tillerson na rais wa nchi hiyo Donald Trump. Sambamba na hatua hiyo, chombo kikuu cha usalama na intelijinsia cha Marekani yaani CIA, nacho pia kimefanyiwa mabadiliko ya msingi kwa hatamu za uongozi wake kukabidhiwa mwanamke kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo. Hayo yote yanadhihirisha ufa mkubwa wa hitilafu na tofauti zilizopo, na kushtadi mivutano katika vyombo vya juu kabisa vya upitishaji maamuzi vya serikali ya Marekani.

Mike Pompeo, aliyeteuliwa kuwa waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani

Suala la kutimuliwa au kujiuzulu Rex Tillerson wadhifa wa uwaziri wa mambo ya nje ya Marekani limekuwa tab'an likizungumziwa na vyombo vya habari tangu miezi kadhaa nyuma. Miezi michache tu baada ya Trump kuingia Ikulu ya White House, tofauti na hitilafu zilianza kujitokeza kati yake na waziri wake wa mambo ya nje. Hitilafu hizo zilikuwa juu ya masuala mengi, kuanzia kadhia ya shirika la kijeshi la NATO na Russia mpaka juu ya namna ya kukabiliana na Iran na Korea Kaskazini. Trump na Tillerson walikuwa wakitafautiana sana pia katika maudhui nyingine kadhaa kama mgogoro wa kidiplomasia wa Qatar, mazungumzo ya mapatano ya Mashariki ya Kati pamoja na mustakabali wa Syria na Afghanistan. Donald Trump, akiwa ni mwanasiasa mwanagenzi na asiye na uzoefu aliyeibukia kwenye vuguvugu la mielekeo ya utaifa, amekuwa akisisitizia kufuatwa sera za kigeni za uchukuaji maamuzi ya upande mmoja, kupinga ushirikishi wa kimataifa na kutetea matumizi ya mkono wa chuma, misimamo ambayo imezusha mgongano na chombo kikuu cha diplomasia cha Marekani ambacho kinatilia mkazo kuendelezwa muelekeo wa kuwa na sera za pamoja na mataifa mengine kimataifa, kuendeleza miungano mikubwa iliyopo na kuyalinda mahusiano yaliyoko katika nidhamu ya kimataifa. Kwa muda fulani ilihisika kwamba moto wa tofauti na mivutano kati ya Trump na Tillerson ungeweza kupoa kwa kiwango fulani kufuatia upatanishi uliofanywa na watu kama Jenerali Herbert McMaster, mshauri wa usalama wa taifa na James Mattis, waziri wa ulinzi wa nchi hiyo.

Rais Donald Trump wa Marekani na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong un

Hata hivyo msimamo na uamuzi aliochukua Trump kuhusiana na moja ya migogoro hasasi na nyeti zaidi katika siasa za nje za Marekani, yaani kadhia ya nyuklia katika Peninsula ya Korea, umeonyesha kuwa kiongozi huyo ameamua kulifunga moja kwa moja faili la tofauti zilizopo kati yake na waziri wake wa mambo ya nje. Saa chache baada ya Trump kutoa kauli ambayo haikutarajiwa, ya kuafiki kukutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong un kwa upatanishi wa Korea Kusini, Rex Tillerson, ambaye alikuwa ziarani barani Afrika alitamka kwamba, mabadiliko hayo makubwa ya kimsimamo ni uamuzi binafsi wa Trump. Vyombo vya habari viliripoti pia kwamba hali ya kiafya ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani haikuwa nzuri na kwa sababu hiyo ameakhirisha baadhi ya ratiba alizokuwa amepangiwa katika safari yake barani Afrika na kwamba atarudi Washington mapema zaidi kwa siku moja. Kurejea Marekani kwa Tillerson kulikwenda sambamba na ujumbe wa twitter wa Trump wa kumtangaza waziri mpya wa mambo ya nje wa nchi hiyo.

Baada ya hayo, zamu sasa ni ya Baraza la Seneti lenye wingi tete wa wajumbe wa chama cha Republican, kuchukua uamuzi kuhusu uteuzi wa waziri mpya wa mambo ya nje na vilevile mkurugenzi mpya wa CIA; kadhia ambayo inavyoonekana, haitopita vivi hivi bila ya kutokea mivutano au mikwaruzano yoyote.../