Nato: Hatutaki vita vipya baridi na Russia
Jens Stoltenberg Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) alisema jana kuwa muungano huo hautaki kurudi katika uhasama wa vita baridi kati yake na Russia huku akibainisha uungaji mkono wake kwa msimamo mkali uliodhihirishwa na Uingereza kufuatia madai kwamba Moscow imempatia sumu jasusi wa zamani wa nchi hiyo huko Uingreza.
Stoltenberg amesema kuwa Nato haitaki kuingia katika vita vipya baridi wala haitaki mashindano mapya ya silaha. Amesema Russia ni jirani ya Nato na kwa msingi huo muungano huo unapasa kuendelea kufanya juhudi za kuboresha uhusiano na Russia. Katibu Mkuu wa Muungano wa Nato ameongeza kuwa muungano huo katika miaka ya karibuni umeiwekea Russia vikwazo vya kiuchumi na kutuma vikosi zaidi mashariki mwa Ulaya ikiwa ni katika kuitikia kile alichokitaja kuwa "hali ya usalama iliyobadilika."
Nato imeiunga mkono Uingereza kufuatia madai ya kutekelezwa shambulio tarehe mwezi huu wa Machi katika mji wa Salisbury kusini magharibi mwa Uingereza; shambulio lililosababisha kuwa katika hali mahututi jasusi wa zamani wa Russia Sergei Skripal na binti yake anayejulikana kwa jina la Yulia. Russia imekanusha kuhusika kivyovyote katika tukio hilo.