Mar 20, 2018 15:53 UTC
  • Msikiti mwingine washambuliwa kwa bomu nchini Ujerumani

Msikiti mmoja katika mji wa Ulm, kusini mwa Ujerumani umeshambuliwa kwa bomu na watu wasiojulikana, chini ya wiki mbili baada ya msikiti mwingine kuteketezwa kwa moto katika mji mkuu wa nchi hiyo ya Ulaya, Berlin.

Duru za habari zinasema kuwa, msikiti huo unaomilikiwa na jamii ya Waislamu wa Kituruki ulishambuliwa jana kwa bomu la petroli na kuharibiwa, ingawaje hakuna visa vya majeruhi vilivyoripotiwa.

Jamii ya Waturuki katika mji huo chini ya mwavuli wa Islamic Community National View (IGMG) imelaani vikali tukio hilo na kulitaja kuwa la kigaidi. Baadhi ya vyanzo vya habari vinasema yumkini mashambulio ya hivi karibuni dhidi ya misikiti nchini Ujerumani yametekelezwa na Kundi la kigaidi la PKK.

Machi 10, katika kile kinachoonekana kuwa ni muendelezo wa matukio ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu barani Ulaya, wavamizi wasiojulikana waliuteketeza moto Msikiti wa Jamia wa Koca Sinan katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin.

Waislamu nchini Ujerumani

Mashambulizi dhidi ya Waislamu na maeneo yao ya ibada na ya shughuli zao mbalimbali, yameongezeka sana katika siku za hivi karibuni sio tu Ujerumani, bali katika nchi nyingi za Magharibi. Mwaka jana, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani ilisema misikiti 91 na vituo vya dini ya Kiislamu vilishambuliwa nchini humo mwaka 2016 pekee.

Genge lenye chuki za kidini lijulikanalo kwa jina la PEGIDA limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Waislamu nchini Ujerumani.

Tags