Merkel: Kujiondoa Marekani katika makubaliano ya JCPOA kutaanzisha vita
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimetangaza kuwa, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amemtahadharisha Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa nchi za Ulaya zitakuwa pamoja na Iran iwapo Marekani itajiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia na Iran ya JCPOA.
Gazeti la Kizayuni la The Times of Israel limeandika kuwa Merkel alimtaarifu Benjamin Netanyahu pambizoni mwa kikao cha karibuni cha Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi huko Davos nchini Uswisi kuwa kujiondoa Marekani katika makubaliano ya JCPOA kwa upande mmoja si tu kutaibua ufa kati ya nchi za Magharibi, Marekani na Israel bali kutasababisha vita.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kansela wa Ujerumani alimweleza Netanyahu kuwa nchi za Ulaya hazina azma ya kukiuka makubaliano hayo ya kimataifa na kwamba kusambaratika kwa makubaliano ya JCPOA ambako kutatoa pigo kwa hadhi ya nchi za Magharibi, kutatatiza zoezi lolote la kutaka kufikiwa makubaliano ya kidiplomasia katika siku za usoni.
Wakati huo huo kanali ya kumi ya televisheni ya utawala wa Kizayuni wa Israel imetangaza kuwa, Angela Merkel amemweleza Waziri Mkuu wa utawala huo kuwa: Kujiondoa Marekani katika makubaliano ya JCPOA kutazifanya Ujerumani, Uingereza na Ufaransa ziwa na msimamo wa pamoja na Russia, China na Iran na kwamba Marekani na Israel zitakuwa katika upande mwingine.
Pande nyingine katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yaani Uingereza, Ufaransa, Russia, China, Ujerumani na Umoja wa Ulaya zimesisitiza mara kadhaa kuwa makubaliano hayo ni ya jamii ya kimataifa na kwamba hayawezi kubadilishwa na upande mmoja.