Trump awafukuza wanadiplomasia 60 wa Russia, Putin asema atalipiza kisasi
Rais Donald Trump wa Marekani amewafukuza makumi ya wanadiplomasia wa Russia walioko nchini Marekani kufuatia kwa kusingizio cha kupewa sumu jasusi wa zamani wa Russia nchini Uingereza.
Trump leo Jumatatu ameagiza kuondoka Marekani wanadiplomasia 60 wa Russia katika kuonyesha mshikamano wake na Uingereza kuhusu madai kwamba Russia ilimpa sumu jasusi wa zamani wa nchi hiyo huko Uingereza, Sergei Skripal. Trump pia ameagiza kufungwa ubalozi mdogo wa Russia mjini Seattle.
Maafisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Marekani wamesema kuwa Warussia wote 60 walikuwa majasusi wakifanya kazi chini ya anwani ya diplomasia; wakiwemo pia wengine zaidi ya kumi na mbili katika ofisi ya balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa. Wamedai kuwa, kufukuzwa kwa wanadiplomasia hao wa Russia kunatuma ujumbe kwa Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo kuhusu idadi kubwa isiyokubalika ya maajenti wa intelijinsia wa Russia wanaofanya kazi nchini Marekani.
Wakati huo huo nchi 14 wanachama wa Umoja wa Ulaya zimeamua kuwafukuza wanadiplomasia kadhaa wa Russia waliopo katika nchi hizo. Hayo yameelezwa leo na Donald Tusk Mwenyekiti wa Baraza la Ulaya. Uamuzi huo ulichukuliwa Ijumaa iliyopita katika mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya.
Serikali ya Russia kwa upande wake imetangaza kuwa itajibu hatua hiyo ya Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya ya kuwafukuza wanadiplomasia wake.
Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin imesema imesikitishwa na hatua hiyo lakini imesisitizia kwamba italipiza kisasi.