NATO: Hatuko katika mashindano ya silaha mpya na Russia
Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) amesema kuwa muungano huo hauko katika mashindano ya silaha mpya na Russia.
Jens Stoltenberg ameyasema hayo katika mazungumzo ya pamoja na Justin Trudeau, Waziri Mkuu wa Canada mjini Ottawa na kuongeza kuwa, NATO haikusudii kushindana na Russia kuhusiana na silaha mpya na badala yake itajitahidi kuwa na mahusiano mema na Moscow. Amesema kuwa, NATO imejiandaa kufanya mazungumzo chanya na viongozi wa Russia. Mgogoro kati ya nchi za Magharibi na Russia ulishika kasi baada ya sakata la kupewa sumu jasusi wa zamani wa Russia Sergei Skripal.
Uingereza na nchi nyingine za Magharibi zinaituhumu Moscow kuwa ilihusika na kitendo hicho, huku viongozi wa Russia wakikanusha kuhusika kwa ajina yoyote na tukio hilo. Katika miaka ya hivi karibuni Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) iliongeza harakati zake za kijeshi katika nchi za eneo la mashariki mwa Ulaya ambazo zinapakana na Russia. Suala hilo liliifanya Moscow kujizatiti na kuweka askari wake katika mpaka na nchi hizo suala ambalo lilizidisha hali ya wasi wasi wa kutokea vita kati ya pande mbili.