White House: Hadi sasa Trump hajachukua maamuzi yoyote kuhusu Syria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i43020-white_house_hadi_sasa_trump_hajachukua_maamuzi_yoyote_kuhusu_syria
Msemaji wa Ikulu ya Marekani (White House) Sarah Huckabee Sanders amesema kuwa, hadi sasa rais wa nchi hiyio Donald Trump hajachukua maamuzi ya mwisho kuhusu Syria, licha ya kufanya kikao na timu ya usalama wa taifa katika ikulu ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 12, 2018 23:40 UTC
  • White House: Hadi sasa Trump hajachukua maamuzi yoyote kuhusu Syria

Msemaji wa Ikulu ya Marekani (White House) Sarah Huckabee Sanders amesema kuwa, hadi sasa rais wa nchi hiyio Donald Trump hajachukua maamuzi ya mwisho kuhusu Syria, licha ya kufanya kikao na timu ya usalama wa taifa katika ikulu ya nchi hiyo.

Trump na timu ya usalama wa taifa ya Marekani wamekutana White House na kujadili chaguo ambalo Marekani inaweza kuchukua dhidi ya Syria. Baadhi ya duru za habari zimeripoti kujiri mvutano mkali kati ya James Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani na John R. Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa ikulu ya White House katika kikao hicho.

Kikao cha Trump kilichoambulia patupu

Kwa mujibu wa habari hiyo, waziri wa ulinzi wa Marekani ameonyesha wasi wasi wake mkubwa juu ya mgogoro unaoweza kuzuka iwapo Marekani itaishambulia Syria na kadhalika madhara yatakayowapata askari wa Marekani. Baada ya kushindwa kufikia mwafaka, leo tena Trump na timu yake hiyo amepanga kufanya kikao kingine kuhusiana na suala hilo. Hayo yanajiri katika hali ambayo Trump na baadhi ya viongozi wa Marekani hivi karibuni walinukuliwa wakitoa matamshi makali ya kwamba wamepanga kuishambulia kijeshi Syria kwa kisingizio cha kutumiwa silaha za kemikali katika eneo la Duma nchini humo, suala ambalo limekadhibishwa vikali na serikali ya Damascus.

Matumizi ya silaha za kemikali, madai bandia yanayotumiwa na madola ya Magharibi dhidi ya Syria

Aidha kituo cha uangalizi wa kijeshi wa jeshi la Russia nchini Syria hivi karibuni kilitangaza kuwa, uchunguzi uliofanyika umebaini kwamba, hakuna shambulizi lolote la silaha za kemikali lililofanyika karibu na mji wa Duma huko Ghouta Mashariki katika viunga vya Damascus, mji mkuu wa nchi hiyo kama ambavyo Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi zimekuwa zikitangaza. Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi zinatoa tuhuma hizo dhidi ya serikali halali ya Syria bila ya kuwa na uthibitisho wowote.