Trump akosolewa kwa kuishambulia Syria bila idhini ya Kongresi
Wabunge wa vyama vya Republican na Democrat nchini Marekani kwa pamoja wametoa radiamali wakimkosoa Rais Donald Trump wa nchi hiyo kwa kuishambulia Syria bila ya kupata idhini ya Kongresi.
Juzi Ijumaa Trump alitangaza kuwa Washington imeanzisha mashambulizi ikishirikiana na Uingereza na Ufaransa dhidi ya maeneo maalumuu huko Syria. Mashambulizi hayo ya anga yalianzishwa eti kujibu kile kinachodaiwa kuwa shambulizi la kemikali lililofanyika katika mji wa Douma tarehe 7 mwezi huu. Nchi za Magharibi ziliituhumu serikali ya Rais Bashar al Assad kuwa ndiyo iliyofanya shambulio hilo la kemikali. Damascus kwa upande wake imekanusha vikali madai hayo na hadi sasa hakuna taasisi yoyote ya kimataifa iliyothibitisha madai hayo.
Masaa kadhaa kabla ya kufanyika mashambulizi ya makombora huko Syria, wawakilishi 87 wa Kongresi ya Marekani walituma barua White House wakimtaka Trump asichukue hatua ya kijeshi bila ya idhini ya kongresi. Hata hivyo Trump ambaye mapema wiki iliyokwisha alitishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Damascus alipuuza barua hiyo na kuamuru Ijumaa kutekelezwa mashambulizi ya anga dhidi ya Damascus.
Wawakilishi hao wa vyama vya Republican na Democrat wamesema kuwa uamuzi huo wa Rais Trump wa kuishambulia Syria bila ya ya kupasishwa na Kongresi ya nchi hiyo ni kinyume cha sheria. Seneta Tim Kaine amesema kuwa iwapo leo hii Trump ameamua kuishambulia Syria, basi kitu gani kitamzuia asizishambulie nchi nyingine bila ya idhini ya Kongres?