UN: Watu 4,000 wamekimbia mapigano mapya Myanmar
Umoja wa Mataifa umesema watu zaidi ya elfu nne wamekimbia mapigano mapya kati ya wanajeshi wa Myanmar na genge moja la kikabila katika muda wa wiki chache zilizopita, kaskazini mwa nchi.
Mark Cutts, Mkuu wa Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, watu zaidi ya elfu nne wamelazimika kuwa wakimbizi katika jimbo la Kachin karibu na mpaka na China, ndani ya majuma matatu yaliyopita.
Zaidi ya watu 15,000 tayari walikuwa wamelazimika kuyakimbia makazi yao katika jimbo hilo, baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya usitishaji vita kati ya jeshi la nchi hiyo na genge la waasi wenye kubeba silaha la Kachin Independence Army (KIA), mwaka 2011.
Jeshi la Myanmar linatuhumiwa kutumia silaha nzito sambamba na kutekeleza mashambulizi ya anga dhidi ya waasi hao wa Kachin, hujuma ambazo zimekuwa zikisababisha mauaji dhidi ya raia wasio na hatia pia.

Hii ni katika hali ambayo, Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopewa jukumu la kutathmini athari za mgogoro wa wakimbizi Waislamu wa Rohingya unajiandaa kuuzuru mkoa wa Rakhine unaopatikana magharibi mwa Myanmar Jumatatu ijayo.
Tangu mwezi Agosti mwaka jana vikosi vya serikali ya Myanmar vimeshadidisha mashambulizi dhidi ya Waislamu waliowachache wa kabila la Rohingya katika eneo hilo, ambapo mbali na maelfu miongoni mwao kuuawa, wengine zaidi ya 700,000 wamelazimika kukimbilia usalama wao katika nchi jirani ya Bangaldesh.