Kutengwa Marekani katika Muungano wa (NATO) juu ya kadhia ya JCPOA
Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO), Jens Stoltenberg ametoa matamshi yanayokinzana na mtazamo wa Rais Donald Trump wa Marekani kuhusiana na makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi sita kubwa za dunia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.
Jens Stoltenberg amesema kuwa masuala ya kieneo na kadhalika kadhia ya makombora ya nyuklia ya Iran hayahusiani na Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA. Katibu Mkuu wa NATO ameyasema hayo baada ya kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa muungano huo wa kijeshi kilichofanyika mjini Brussels, Ubelgiji wakati akijibu swali lililoulizwa na mwandishi wa habari kuhusiana na kukamilika makubaliano hayo ya nyuklia kwa kutegemea makubaliano mengine mapya ambapo alisema: "NATO inaunga mkono tu utekelezwaji wa makubaliano hayo." Mwisho wa kunukuu.
Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) na ambao ni nguvu ya kijeshi ya Marekani barani Ulaya una mahusiano ya karibu na siasa za Washington kuhusiana na masuala mbalimbali ya usalama wa dunia. Pamoja na hayo muungano huo ambao bajeti yake kuu inadhaminiwa na serikali ya Marekani, umetupilia mbali mitazamo hasi ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ni katika hali ambayo Trump ametishia kwamba hadi kufikia tarehe 12 Mei mwaka huu iwapo hakutafanyika mabadiliko katika siasa za makombora ya Iran au kuhusiana na siasa za eneo, basi ataiondoa nchi yake katika makubaliano hayo. Vitisho dhidi ya makubaliano ya kimataifa ambayo uwepo wake umepitishwa pia na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ni suala ambalo limeutia ulimwengu wasi wasi mkubwa. Wasi wasi huo hauishii tu kwa nchi zinazojitegemea au washindani wa Marekani, bali umewatia tumbo joto hata washirika wakubwa wa kisiasa na kijeshi wa Washington hasa kutokana na matokeo mabaya yakatayopatikana baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano hayo ya nyuklia.
Katika uwanja huo msimamo wa Katibu Mkuu wa NATO ni wenye kuzingatiwa sana. Hata hivyo isisahaulike kwamba mtazamo wa Jens Stoltenberg ndio msimamo wa aghlabu ya nchi washirika wa muungano huo wa kijeshi wa nchi za Magharibi. Miongoni mwa wanachama 29 wa nchi za NATO ni Marekani pekee ambayo imeyaona makubaliano hayo ya nyuklia kuwa yasiyo na maana. Hii ni katika hali ambayo makubaliano hayo ambayo yalipatikana baada ya juhudi kubwa na kwa muda mrefu yakizihusisha nchi nne wanachama wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) yaani Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani na nchi tatu nyingine yaani Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia na China, yalifikiwa kupitia fremu ya waraka wa kurasa 150. Baada ya hapo waraka huo uliungwa mkono na nchi tatu zenye haki ya kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani Marekani, Ufaransa na Uingereza.
Hii ni kusema kuwa hadi sasa na baada ya zaidi ya miaka miwili tangu kuanza kutekelezwa makubaliano hayo ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA, Trump amekusudia kuanzisha mgogoro mpya duniani kuhusiana na suala hilo. Viongozi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameweka bayana kwamba, iwapo Marekani itaamua kujiondoa katika makubaliano hayo, basi Tehran itafufua miradi yake ya nyuklia kwa kasi kubwa. Kwa hakika suala hilo ni kengele ya hatari kwa asasi tofauti kama vile Umoja wa Ulaya ambao ni mshirika mkubwa wa Marekani, kisisa, kiuchumi na kijeshi.
Kuhusiana na suala hilo Medea Benjamin, mwanaharakati anayepinga vita wa nchini Marekani anasema: "Ikiwa Marekani na kwa mujibu wa madai ya Rais Donald Trump itaamua kujiondoa katika makubaliano hayo ya nyuklia ya Iran, basi kuna uwezekano kwa mara nyingine dunia ikaelekezwa kwenye vita hatari sana katika eneo la Mashariki ya Kati na ni kwa msingi huo ndio maana kambi ya Ulaya, Kongresi ya Marekani na hata fikra za walio wengi nchini humo zikawa na nafasi muhimu kwa ajili ya kuzuia hali hiyo." Mwisho wa kunukuuu. Pamoja na hayo hadi sasa hakuonekani uwezekano wa Trump kuikinaisha dunia ukiwemo muungano wa NATO kuhusiana na suala la kuiondoa nchi yake katika makubaliano ya nyuklia ya Iran. Suala hilo linaonyesha kwamba harakati ya kitaifa nchini Marekani na inayoongozwa na Trump hazizingatii asasi tofauti ukiwemo Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO).