WHO: New Delhi ndio mji wenye hewa chafu zaidi duniani
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza katika ripoti yake mpya kuhusu kiwango cha usafi wa hewa katika miji mikubwa duniani na kuutaja mji mkuu wa India New Delhi kuwa ndio wenye hewa chafu zaidi duniani.
Ripoti hiyo ya WHO imeeleza kuwa vumbi na ukungu mchafu, utitiri wa vyombo vya usafiri wa barabarani, moshi uliotanda kutokana na fueli ya fosili pamoja na kukithiri idadi ya watu vimeufanya mji mkuu wa India, New Delhi uongoze katika miji yenye hewa chafu zaidi duniani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mji mkuu wa Misri, Cairo ni wa pili kwa hewa chafu zaidi duniani ukifuatiwa na mji mkuu wa Bangladesh Dhaka na Mumbai ambao ni mji mkuu wa kibiashara wa India.
Nafasi ya tano ya miji mikubwa yenye hewa chafu zaidi duniani inashikiliwa na mji mkuu wa China, Beijing.
Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Afya Duniani kuhusu kiwango cha chembechembe za ukungu mchafu uliotanda kwenye anga ya hewa unaonyesha kuwa asilimia 90 ya watu duniani wanakabiliwa na hatari ya kuvuta hewa chafu na kwamba hali hiyo ilisababisha vifo vya watu milioni sita katika mwaka 2016.
Taasisi ya Kimarekani iitwayo "Athari za Siha" nayo pia ilitoa ripoti mnamo mwezi uliopita wa Aprili na kutangaza kuwa katika mwaka huu wa 2018 zaidi ya nusu ya vifo vinavyosababishwa na hewa chafu vitatokea katika nchi za India na China.../