Marekani yawalaumu Wapalestina kwa kuuawa na askari wa Israel, Gaza
Ikulu ya Marekani White House imejitokeza kuutetea hadharani utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuwaua shahidi Wapalestina wasiopungua 54 waliokuwa wakishiriki maandamano katika Ukanda wa Gaza siku ya Jumatatu.
Raj Shah, Naibu Katibu wa Vyombo vya Habari wa Ikulu ya White House amesema jeshi la Israel lilikuwa na kila haki ya kujilinda baada ya kuchokozwa.
Amesema, "Tunaamini Hamas ndiyo inayopaswa kubeba dhima kwa yale yote yaliyotokea, wao ndio waliochochea ghasia hizo wakitambua kuwa kungekuwako na umwagikaji damu."
Mbali na makumi kuuawa, Wapalestina wengine zaidi ya 2,700 walijeruhiwa katika mauaji hayo ya umati ambayo yalitekelezwa na askari wa utawala katili wa Israel.
Wapalestina hao waliuawa kikatili kwa kushiriki 'Maandamano ya Haki ya Kurejea", yaliyofanyika kwa lengo la kulaani vikali na kupinga hatua ya Marekani kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi mji wa Quds Tukufu au Jerusalem.
Tokea Machi 30 Wapalestina wamekuwa wakishiriki katika maandamano hayo ya 'Haki ya Kurejea' kila Ijumaa ambapo hadi sasa karibu Wapalestina 53 wameuawa tangu wakati huo hadi Mei 13, kwa kufyatuliwa risasi na wanajeshi wa Israel katika maadanamano hayo ya amani ambayo hufanyika katika mpaka wa Gaza na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.