Maelfu ya Wamarekani waandamana kupinga uhuru wa kutembea na bunduki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i45380-maelfu_ya_wamarekani_waandamana_kupinga_uhuru_wa_kutembea_na_bunduki
Maelfu ya Wamarekani wameandamana katika mji wa New York kupinga na kulalamikia uhuru wa raia kutembea na bunduki nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 03, 2018 23:43 UTC
  • Maelfu ya Wamarekani waandamana kupinga uhuru wa kutembea na bunduki

Maelfu ya Wamarekani wameandamana katika mji wa New York kupinga na kulalamikia uhuru wa raia kutembea na bunduki nchini humo.

Washiriki wa maandamano hayo waliokuwa wakitoa sha'ar na miito ya shime walibeba mabango yenye maandishi ya kulaani ukatili unaofanywa nchini humo kwa kutumia silaha moto.

Waandamanaji hao aidha wamesema uzembe unaofanywa wa kutochukua hatua za kulinda mfumo wa elimu wa shule za serikali na uhaba wa bajeti inayohitajika kwa ajili ya kuzuia kutokea matukio ya ukatili na utumiaji nguvu unaohusiana na ubebaji silaha ni miongoni mwa sababu za kushamiri ukatili na mauaji nchini humo.

Maandamano hayo yamefanyika baada ya kupita karibu wiki mbili tangu lilipotokea shambulio la ufyatuaji risasi lililofanywa na mwanafunzi mmoja katika skuli ya Sante Fe iliyoko kwenye jimbo la Texas. Wanafunzi tisa na mwalimu wao waliuawa na wengine kumi walijeruhiwa katika shambulio hilo.

Rais wa Marekani Donald Trump ni muungaji mkono mkubwa wa uhuru wa raia kutembea na bunduki

Kabla ya hapo pia mnamo mwezi Februari mwaka huu, watu 17 waliuawa na makumi ya wengine walijeruhiwa katika shambulio jengine la ufyatuaji risasi lililofanywa katika skuli ya Stoneman Douglas iliyoko mjini Parkland katika jimbo la Florida.

Kuongezeka matukio ya umwagaji damu ya mashambulio ya ufyatuaji risasi nchini Marekani hususan katika skuli za nchi hiyo kumepelekea kufanyika maandamano mengi na makubwa yanayoshirikisha wanafunzi na wanaharakati wanaopinga uhuru wa kutembea na bunduki nchini humo.../