EU: Hatua ya Iran ya kuimarisha urutubishaji urani haikiuki JCPOA
Umoja wa Ulaya umesema tathmini yake ya mwanzo inaashiria kuwa mpango wa Iran wa kuimarisha urutubishaji urani hadi kufikia kiwango cha SWU 190,000 haukinzani na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Maja Kocijancic, msemaji wa Mkuu wa Sera za Nje za EU, Federica Mogherini ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, uamuzi huo wa Iran haukiuki hata kidogo makubaliano ya nyuklia ya Iran yaliyoanza kutekelezwa Januari mwaka 2016.
Hata hivyo amedai kuwa, hatua hiyo ya Iran wakati huu haitakuwa na mchango chanya katika kujenga imani kuhusu mradi wake wa nyuklia.
Hapo jana Msemaji wa Shirika la Atomiki la Iran Behrouz Kamalvandi, lisema Iran imeufahamisha Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuwa imeanzisha mchakato wa kuimarisha uwezo unaohitajika wa kuzalisha gesi aina ya UF6 na UF4 na ujenzi wa kiwanda cha kutengenza mashinepewa (centrifuge), mambo yanayohitajika kwa ajili ya kurutubisha madini ya urani yanayotumika katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia.
Katika hotuba yake Jumatatu iliyopita katika maadhimisho ya mwaka wa 29 tokea alipoaga dunia Imam Khoemini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Kiongozi Muadhamu alitoa amri kwa Shirika la Atomiki la Iran na kusema: "Matayarisho yanayohitajika kwa ajili ya kufikiwa kiwango cha SWU 190,000 yaanze kutekelezwa haraka katika fremu ya mapatano ya JCPOA."
Katika hatua nyingine, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema hakuna kiashiria chochote kinachoonyesha kuwa Iran inakiuka makubaliano ya JCPOA. Macron aliyasema hayo jana katika kikao na waandishi wa habari akiwa pamoja na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambaye anafanya safari katika nchi za Ulaya kuzishawishi zijiondoe kwenye mapatano hayo ya kimataifa.