Waziri wa Vita wa Israel atoa matamshi ya kijinga kumhusu Messi
Waziri wa Vita wa Utawala wa Kizayuni wa Israel ametoa matamshi ya kijinga sana kumuhusu nyota wa timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi baada ya timu yake kutoka sare na Iceland katika kombe la dunia nchini Russia.
Katika mechi hiyo ya jana Jumamosi, Messi alikosa mkwaju wa penalti na hatimaye timu hizo mbili zikatoka sare ya bao moja kwa moja na hivyo Argentina ikapata pointi moja.
Kufuatia matokeo hayo, Waziri wa Vita wa Utawala wa Kizayuni wa Israel Avigdor Lieberman ametoa matamshi ya kijinga kumhusu Messi na kusema: "Iwapo Argentina ingecheza mechi ya kirafiki na Israel, Messi angekuwa na uwezo bora zaidi katika kombe la dunia. Messi amepoteza penalti hiyo kwa sababu hakuwa amejitayarisha vya kutosha."
Ikumbukwe kuwa kufuatia mashinikizo makubwa ya kimataifa na malalamiko makali ya Wapalestina na waungaji mkono wa ukombozi wa Palestina kote duniani, mechi ya kirafiki kati ya timu ya taifa ya Argentina na timu ya utawala wa Kizayuni iliyokuwa ichezwe Juni tisa nchini Cyprus ilifutiliwa mbali.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, kipa wa Iceland Hannes Halldorsson amesema kabla ya mechi hiyo ya jana alichukua muda mrefu sana kuchunguza namna Messi anavyopiga mikwaju ya penalti na hivyo akafanikiwa kuzuia penalti hiyo.
Timu ya Iceland pia ilipata umaarufu mwaka 2016 baada ya kuichapa England mabao mawili kwa moja na hivyo kuindoa katika mashindano ya kombe la Ulaya.