UN: Wahajiri 1,400 wamekufa maji tangu Januari mwaka huu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46612-un_wahajiri_1_400_wamekufa_maji_tangu_januari_mwaka_huu
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema zaidi ya wahajiri 1,400 wamefariki dunia katika Bahari ya Mediterania tangu ulipoanza mwaka huu wa 2018 hadi sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 06, 2018 22:57 UTC
  • UN: Wahajiri 1,400 wamekufa maji tangu Januari mwaka huu

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema zaidi ya wahajiri 1,400 wamefariki dunia katika Bahari ya Mediterania tangu ulipoanza mwaka huu wa 2018 hadi sasa.

Charlie Yaxley, msemaji wa shirika hilo la UN amesema ingawaje safari za wahajiri za kuelekea barani Ulaya zimepungua, lakini idadi ya vifo inaonekana kuongezeka kwa kiasi kikubwa.

Taarifa ya UNHCR imeeleza kuwa, wahajiri hao wamekufa maji wakiwa katika juhudi za kuelekea barani Ulaya kutokea Libya, kwenda kutafuta maisha wanayosema ni mazuri.

Amesema wahamiaji wanaokwenda kutafuta hifadhi na wahajiri wapatao 46,000 wamewasili katika nchi za bara Ulaya za Italia na Malta kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa; ikiwa ni mara tano chini ya kiwango kilichoshuhudiwa mwaka 2016.

Wakati huo huo, Ofisi ya Shirika la Kimataifa la Uhajiri (IOM) nchini Libya  imesema kuwa, idadi ya wahajiri wanaopoteza maisha katika pwani ya nchi hiyo imeongezeka kwa kiwango cha kutisha.

Wahajiri wa Kiafrika wakinusuriwa

Itakumbukwa kuwa, hivi karibuni viongozi wa nchi za Ulaya  walikubaliana kuwahamishia kaskazini mwa Afrika wakimbizi na wahajiri haramu wanaoelekea barani Ulaya kupitia bahari ya Mediterania. 

Hata hivyo nchi tano za kaskazini mwa Afrika zilikataa mapendekezo ya viongozi wa Ulaya ya kuanzisha kambi maalumu za wahajiri katika ardhi za nchi hizo kwa ajili ya kuwapokea wahajiri wa Kiafrika.

Nchi za EU zimekuwa zikivutana kuhusu mgogoro huo wa wahajiri haswa wanaotokea barani Afrika kupitia Libya.