Jul 24, 2018 16:20 UTC
  • Erdogan: Israel ndio utawala wa kifashisti na kibaguzi zaidi duniani

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameutaja utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ndio utawala wa kifashisti na wa kibaguzi zaidi duniani.

Sanjari na kulaani sheria ya kibaguzi iliyopasishwa hivi karibuni na Bunge la Israel, Erdogan amesema kupasishwa kwa sheria hiyo kunaashiria kufufuka kwa mizimu ya Hitler kwenye nyoyo za watawala wa Israel, akisisitiza kuwa, binafsi haoni tofauti yoyote kati sera za utawala haramu wa Israel na sheria za kinazi za Ujerumani enzi za dikteta Adolf Hitler.

Alkhamisi iliyopita Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) lilipasisha muswada wa sheria inayotaka kutambuliwa Israel kama 'dola la Mayahudi pekee' licha ya upinzani mkali na malalamiko kutoka kila pembe ya dunia, licha ya mashirika ya kutetea haki za binadamu kufanya maandamano nje ya bunge hilo wakiipinga sheria hiyo.    

Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset)

Taasisi mbalimbali za kimataifa ikiwemo Jumuiya ya Mabunge ya nchi wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Harakati ya Hizbullah ya Lebanon na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zimelaani hatua ya kupasishwa sheria hiyo ya 'apartheid'.

Kadhalika Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu kupitishwa kwa sheria hiyo ya ubaguzi wa rangi na kusema kuwa inapingana moja kwa moja na maazimio ya umoja huo.

Tags