Gazeti la Haaretz: Israel inashiriki katika mauaji ya Waislamu Warohingya
Gazeti la Haaretz la Israel limefichua kuwa, utawala haramu wa Israel umetiliana saini mikataba ya uuzaji silaha na serikali ya Myanmar na kwamba, umekuwa ukishiriki katika mauaji dhidi ya Waislamuu Warohingya katika jimbo la Rakhine.
Ufichuaji wa karibuni kabisa wa gazeti la Haaretz unaeleza kwamba, hatua ya Israel ya kutiliana saini mikataba ya uuzaji silaha na serikali ya Myanmar imefunua pazia la nafasi ya Tel Aviv katika kuangamiza kizazi cha Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar.
Gazeti hilo limeashiria ripoti ya hivi karibuni ya Kamati ya Kutafuta Ukweli ya Umoja wa Mataifa ambayo ilitoa nyaraka na ushahidi kuhusu kuuawa na jeshi la Myanmar Waislamu Warohingya na kukiri kwamba, ripoti hiyo haijitaka Israel isitishe ushirikiano wake na Myanmar kwa kuacha kuiuzia silaha nchi hiyo.
Septemba 2015, Jenerali Min Aung Hlaing, Mkuu wa Jeshi la Myanmar alifanya safari Tel Aviv Israel ambapo mbali na kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa utawala huo, pande hizo mbili zilitiliana saini mkataba wa Myanmar kununua silaha kutoka Israel uliokuwa na thamani ya makumi ya mamilioni ya dola.
Hivi majuzi Kamati ya Kutafuta Ukweli ya Umoja wa Mataifa nchini Myanmar ilisema katika ripoti yake kwamba, kuna udharura wa kufanyika uchunguzi mkubwa kuhusu majenerali wa ngazi za juu wa jeshi la Myanmar akiwemo Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo Jenerali Min Aung Hlaing na kuwafungulia mashtaka ya kufanya mauaji ya umati katika jimbo la Rakhine, kufanya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu dhidi ya Waislamu wa Rohingya.