Wageni waendelea kushambuliwa nchini Ujerumani
Wakuu wa jimbo la Saxony la nchini Ujerumaini wametangaza habari ya kuendelea mashambulizi ya magenge ya wabaguzi wa rangi dhidi ya maeneo ya mji wa Chemnitz wa mashariki mwa nchi hiyo.
Televisheni ya France 24 imewanukuu wakuu wa jimbo hilo wakisema jana (Jumamosi) kwamba, magenge ya wabaguzi hao yameshambulia maeneo mbalimbali ya mji wa Chemnitz baada ya kutokea machafuko na fujo siku kadhaa zilizopita.
Wafuasi wa magenge ya ubaguzi wa rangi wamefanya maandamano hayo kuitikia mwito uliotolewa kwa pamoja na vyama vya mrengo wa kulia vyenye misimamo mikali vinavyojulikana kwa kifupi kama AfD pamoja na genge la kupiga vita Uislamu linalojulikana kwa jina la Pegida.
Bi Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani na Heiko Maas, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo wamelaani vitendo hivyo vya kibaguzi vinavyoendeshwa na magenge hayo.
Unyanyasaji na mashambulizi ya magenge ya mrengo wa kulia yenye chuki dhidi ya wageni hasa Waislamu yameongezeka sana katika miezi ya hivi karibuni nchini Ujerumani.
Mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani ilitoa ripoti na kusema kuwa, watu 33 walijeruhiwa katika hujuma za magenge ya kibaguzi mwaka 2017 na kwamba mashambulizi 60 kati ya matukio yote hayo yaliilenga moja kwa moja misikiti.